Header Ads

ad

Breaking News

Wenye Viwanda watakiwa kuchangamkia maonyesho ya EXPO 2025

Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) Leodegar Tenga,akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu wa maonyesho hayo leo Aprili 24,2025 jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WENYE viwanda na makampuni mbalimbali nchini wameshauriwa kuchangamkia maonyesho ya kimataifa ya EXPO 2025 yanayotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) Leodegar Tenga wakati wa uzinduzi wa msimu wa maonyesho hayo.

Alisema malengo ya maonyesho hayo ni kuonyesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.

Alisema EXPO 2025 itasaidia kuonyesha fursa za maendeleo ya viwanda yaliyopo ili kuendelea kuvutiwa uwekezaji wa nje na kukuza viwanda vya ndani ikiwemo kupata wabia wa nje ya nchi.

“Rais amefanyakazi kubwa sana kwenye miaka yake minne amevutia uwekezajiwa pande zote duniani, tumeona mitaji inakuja kutoka nje, teknolojia mpya kwa hiyo nawahamasisha wenye viwanda waje kwenye maonyesho waonyeshe bidhaa zao,” alisema Tenga

Alisema (CTI),inashirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).

Maonyesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Novemba mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam na yanatarajiwa kuhudhuriwa na waonyeshaji 4,000 na watembeleaji zaidi ya 35,000.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Serera amesema Tanzania inazidi kupanda chini ya uongozi shupavu na wenye maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Serikali kuendelea kutekeleza mageuzi ya kina ili kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani, shirikishi na unaoendeshwa na teknolojia.

“Tunawekeza kwenye miundombinu. Tunafanya nishati ya kisasa, kuwezesha biashara, na kuweka dijitali. Tunapunguza gharama za kufanya biashara na kufanya kazi bila kuchoka ili kuiweka Tanzania kama kitovu cha viwanda kwa Afrika Mashariki na Kusini,” alisema.

Amesema marekebisho yaliyofanyika siyo ya mapambo kwani yanalenga kufungua fursa, kuvutia uwekezaji, na kutoa kazi zenye staha kwa watanzania.

Amesema sekta ya viwanda nchini Tanzania inakua na uwekezaji mkubwa umeendelea katika usindikaji wa mazao ya kilimo, vifungashio, dawa, nguo, vifaa vya ujenzi, na hata vifaa vya elektroniki.

“Kupitia Mkakati Jumuishi wa Maendeleo ya Viwanda (IIDS), FYDP III, na marekebisho ya udhibiti, tunaendelea kuweka kipaumbele katika ukuaji wa viwanda kama njia ya ukuaji jumuishi na ushindani wa kimataifa,” alisema.

Afrika sio tena bara la malighafi bali ni bara la masoko na watengenezaji wa bidhaa na kwamba kwa kuwa soko huru la Afrika AfCFTA linatumika sasa, watengenezaji wa bidhaa Tanzania wanaweza kufikia watumiaji bilioni 1.4 katika bara zima.

“Lakini ufikiaji pekee hautoshi lazima tuzalishe kwa kiwango kikubwa, chapa iliyo bor na kuuza nje kwa mkakati ndiyo maana TIMEXPO ni muhimu kwaajili ya kuuambia ulimwengu kwamba kuna bidhaa zinatengenezwa Tanzania. Kama Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kusema: “Tanzania si maskini namimi leo nasema sisi ni matajiri,” alisema.


No comments