WAZIRI MAVUNDE ATOA SIKU 21 TUME YA MADINI KUPITIA MFUMO WA BIASHARA YA MADINI NDANI YA UKUTA MIRERANI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameielekeza Tume ya Madini kupitia upya mfumo wa biashara ya madini ndani ya ukuta wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, ili kuja na pendekezo bora zaidi la namna ya usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini ya Tanzanite kwa lengo la kuongeza thamani ya madini hayo ya kipekee na kuongeza manufaa kwa taifa.
Ameyasema hayo Aprili 24, 2025, wakati wa kikao maalum na viongozi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) kilichofanyika jijini Dodoma kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu biashara ya madini nchini, kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara hao.
“Mkapitie kwa uwazi na uadilifu mkubwa ili kwa pamoja tuje na pendekezo la kuboresha biashara ya madini ya vito ya Tanzanite. Lakini kubwa zaidi ni mkakati wa kuongeza thamani ya madini yetu ya Tanzanite ambayo hayapatikani kwingine duniani isipokuwa hapa Tanzania. Nawapa siku 21 kuanzia leo (Aprili 24, 2025) hadi Mei 15, 2025, mje na ripoti kuhusu mfumo bora wa biashara hii,” amesema Waziri Mavunde.
Katika kuwawezesha wafanyabiashara wa madini nchini, Waziri Mavunde amesema kuwa kupitia mfuko wa dhamana (Credit Guarantee Scheme), Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na TAMIDA, itawachagua baadhi ya wafanyabiashara wa madini kunufaika na mfuko huo. Ikiwa utekelezaji wake utaonesha mafanikio, utaratibu utatengenezwa ili wengine nao waweze kunufaika na mfuko huo kwa lengo la kuinua shughuli zao.
Aidha, Mavunde amemuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Madini kuandaa utaratibu wa utoaji wa leseni mpya kuanzi Julai Mosi, 2025 kwa masonara ili kuondoa changamoto inayowakabili katika kupata malighafi za madini ya vito na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani kwa mawe yasiyo na thamani kubwa.
Vilevile, Mhe. Mavunde amemuelekeza Kamishna wa Madini kwa kushirikiana na TAMIDA kukutana na Kamishna wa Kazi ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wataalam wa uongezaji thamani madini kutoka nje ya nchi, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu katika eneo hilo ili kupata wataalamu wengi wazawa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, ameeleza umuhimu wa kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi ili kulinda ajira za Watanzania na kuimarisha masoko ya ndani na ya kimataifa kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii.
No comments