PONDEZA FOUNDATION WACHANGIA VIFAA VYA UJENZI WA MADRASA YA SHEHIA YA BANKO
Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Taasisi ya Pondeza Fondation, Alhaj, Ussi Salum Pondeza amesema mashindano ya kusoma na kuhifadhi Qur-ani yamekuwa na mchango mkubwa wa kutengeneza jamii bora hapa duniani na kesho Akhera.
Alhaj, Pondeza ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, alitoa kauli hiyo alipojumuika na waislamu mbali mbali katika mashindano ya kuhifadhi Qur-ani yaliyoandaliwa na Jumuiya ya vyuo vya Qur-ani jimbo la Chumbuni, yaliyofanyika Skuli ya Secondary ya Dk. Salmin Amour.
Amewapongeza walimu wanaowasimamia wanafunzi hao na kusema kuwa wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kukuza vipaji vya elimu ya dunia itakayowasaidia wao na vizazi vijavyo.
"Niwapongeze walimu wa madrasa kwa hatua hii kubwa ya kukuza elimu kwa wanafunzi, wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa kujitolea ili kusambaza dini ya Allah (S.W)
Pondeza, amechangia vifaa vya ujenzi kama vile mabati, mbao, misumari, matofali na mchanga kwa ajili ya ujenzi madrasa, iliyopo shehia ya Banko.
Naibu Katibu wa Jumuiya ya vyuo vya Qur-ani Jimbo la Chumbuni, Juma Saleh amesema moja ya mafanikio ya jumuiya hiyo ni kuwa na muendeleo wa kuyafanikisha mashindano kwa kila mwaka toka kuanzishwa kwake 2009.
"Mashindano haya yamekuwa endelevu toka kuanzishwa kwakwe na yalianza kwa hatua ndogo na sasa yamekuwa yakijumuisha hadi juzuu 30," alisema Naibu Katibu.
Alisema, licha ya mafanikio hayo, pia wanakabiliana na changamoto ya kukosa usajili wa jumuiya hiyo hali inayosababisha kukosa kutambulika kwa ngazi ya Jimbo, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Jumla ya washiriki 36 wameshiriki mashindano hayo ya kusoma na kuhifadhi Qur-ani kuanzia Juzuu 1, 3, 5, Juzuu 10, 15, 20 na Juzuu 30 ambapo washindi walikabidhiwa zawadi ya fedha taslim.
No comments