Dkt.Nchimbi azindua kampeni, asema mtaji wa CCM ni imani ya watanzania
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema CCM inaingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa na imani kubwa ya watanzania kutokana na uimara wa chama na uongozi wa Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt.Nchimbi amesema kuwa, uimara wa CCM unatokana na wingi na umakini wa wanachama wake, akitoa takwimu jinsi wanachama wapatao milioni 8 wa CCM walivyojitokeza kupiga kura wakati wa mchakato wa ndani ya chama hicho kupata wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Balozi Nchimbi amesema mtaji wa imani ya watanzania, utumishi wa CCM kupitia sera zake, na uongozi makini unakipatia chama hicho uhakika wa ushindi mkubwa wa kishindo katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
Katibu Mkuu huyo wa CCM ameyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mwanza, uliofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Novemba 27,2024.
Katika kujihakikishia ushindi huo wa kishindo, Balozi Nchimbi amesisitiza kampeni za kuomba kura ziwalenge wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani, ili kuhakikisha kila kura inapatikana kwa ajili ya CCM, akiwahamasisha kupiga kampeni “nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu” nchi nzima.“Pamoja na uhakika wa kura, msiridhike na ushindi. Twendeni nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu. Tusiache kura hata moja. Kila mwanachama atafute kura 10. Hata wa vyama vya upinzani, wawe ACT, NCCR, Chadema na wote, watatupigia kura. Tumalizeni huu mchezo kwa kuipatia CCM ushindi mkubwa wa kishindo.
“Wajibu wetu ni kuwakumbusha tu watanzania kazi kubwa ambayo CCM imeendelea kufanya katika kutoa uongozi wa nchi hii. Uhakika wa kesho ya Tanzania uko CCM.
"Watanzania wana imani kubwa na CCM kila wanapofikiria maendeleo, umoja wa nchi yetu, utaifa wetu, amani na utulivu. Tunataka wagombea wetu mtakapochaguliwa mkalinde heshima na imani hii ya watanzania kwa kuwatumikia vizuri, mkijiepusha na dhuluma na rushwa,”amesema Balozi Nchimbi.
Amesisitiza kuhusu uimara wa CCM, Dkt.Nchimbi anasema CCM ndiyo chama pekee ambacho wanachama wake, kwa mamilioni, walijitokeza kushiriki mchakato wa ndani wa kupata wagombea, hasa kupitia kura za maoni.Ameongeza kuwa, hiyo ndiyo sababu kimesimamisha wagombea maeneo yote nchi nzima katika uchaguzi huo, kwa kuwa kimeenea nchi nzima, tofauti na vyama vingine vya upinzani.
Makalla
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Makalla amesema 4R za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan zitatumiwa na chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.
Makalla ametoa kauli hiyo Novemba 20, 2024 wilayani Temeke wakati akizindua kampeni za CCM kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Sisi kama chama chenye dhamana na ustawi wa maisha ya watanzania, katika uchaguzi huu ambao leo (juzi), tunazindua rasmi kampeni zetu nchi nzima, tumejipambanua kwenda na 4R za Mwenyekiti wa chama chetu Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa sababu tumebeba dhamana kubwa kwa watanzania"amesema Makalla.
Jokate
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jokate Mwegelo (MNEC), amezindua rasmi kampeni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ndani ya Kata ya Bungu wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Jokate amewahamasisha wana CCM kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo.
Katibu huyo wa UVCCM amewapokea wanachama wapya zaidi ya 50 waliotoka vyama vya upinzani wakiwemo wagombea wa nafasi ya mwenyekiti wa kijiji, ambapo wanachama hao wapya wamekiri kusimama kikamilifu na kuwapigia kura wagombea wote wa CCM na kuhakikisha vijiji vyote na vitongoji vinaondokana na siasa za upinzani.
Jokate katika hotuba yake anahimiza zaidi juu ya ushirikiano, umoja na mshikamano katika kutafuta ushindi wa kishindo kwa CCM, hii ni pamoja na kuwasihi kuzingatia Tamko la Uchaguzi lililotolewa kama dira kulekea Novemba 27,2024.
Amewasisitiza wana Kibiti kuendelea kumuunga Mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyoweza kuitekeleza Ilani ya CCM ya 2020/25 na anavyoendelea kukiongoza vyema Chama Cha Mapinduzi na serikali kwa ujumla.
Gavu
Katibu wa Halmashauri Kuu ( NEC) Oganaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu Issa Gavu, amewataka wananchi wa Mkoa wa Geita kuwachagua wagombea wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajia kufanyika Novembe 27, mwaka huu nchini.
Gavu ametoa kauli hiyo Novemba 20,2024 mbele ya mamia ya wananchi wakiwemo wanachama wa CCM alipokuwa akizindua rasmi kampeni za uchaguzi huo, ambapo chama hicho pia kimezindua kampeni zake nchini kote.
“Nawaomba wananchi wa Geita na wanachama wa CCM, kuchagua wagombea wanaotokana na chama chetu ili kusukuma mbele maendeleo yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan.”
Gavu pia amewaomba wagombea kunadi maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita katika maeneo yao na kusisitiza wagombea wanayo nafasi ya kuyaelezea mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020-2025.
Biteko
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko amewataka wananchi wa Nyamongo na Mkoa wa Mara kwa ujumla kufanya kampeni za kistaarabu na kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika Novemba 27, 2024.
Dkt.Biteko ameeleza kuwa, maendeleo hayaletwi kwa matusi wala kuvunjiana heshima na kuwa wananchi hao washinde ubaya kwa wema. Aidha, wamefika eneo hilo kwa lengo la kuwaomba wananchi wa Nyamongo wachague watu ambao wataungana na serikali katika kuwaletea maendeleo.
Dkt.Biteko ameyasema hayo Novemba 20, 2024 wakati akifungua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mara zilizofanyika katika Uwanja Nyamongo Wilaya ya Tarime.
“Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi mkubwa wa kumchagua mtu atakayejua hali na maisha ya watu katika ngazi ya mtaa na ambaye atabeba shida za watu na kuzitatua.”
Amebainisha kuwa, uchaguzi huo ni muhimu na siyo wa majaribio hivyo, ni lazima wananchi wachague viongozi ambao siyo walalamikaji na kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi bali kwa kufanya kazi.
“CCM tumekuja hapa kuwaomba kura zenu, si tu kwa sababu huu ni msimu wa kuomba kura umefika, tumeifanya na tuna cha kuonesha mtakumbuka mwaka 2020 tulikuja na ilani na kusema tutakayoyafanya na tumeeleza hapa tuliyoyafanya,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amesema kuwa, licha ya kufanya siasa ni lazima viongozi wajue wajibu wao ni kuwaletea wananchi maendeleo akitolea mfano namna kijiji kilivyolipwa shilingi bilioni nne ikiwa ni fidia kwa wananchi.
Amefafanua kuwa, Rais Samia ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kuwa na maisha nafuu hivyo, wananchi wa Nyamongo wamuunge mkono kwa kuchagua wagombea wa CCM.
Dkt.Biteko amesema kuwa, kuna fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa jamii (CSR) zinazohitaji kibali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kwamba, amemwelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuhakikisha zinapatikana ili wananchi wa eneo hilo waweze kunufaika kwa kupata miradi ya maendeleo.
Hapi
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, amewataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuacha kulalamika na badala yake kuelekeza nguvu zao katika kuwasilisha na kueleza ajenda za maendeleo kwa wananchi.
Hapi ametoa kauli hiyo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, huku akisisitiza umuhimu wa siasa za hoja zenye tija kwa maendeleo ya taifa, na kusema malalamiko ya mara kwa mara hayaleti manufaa yoyote kwa wananchi, kwani wananchi hawahitaji kusikia porojo wanataka maendeleo.
Hapi anaongeza kuwa, badala ya kuendelea kulalamika, vyama vya upinzani vinapaswa kuonesha mfano kwa kueleza mipango na mikakati yao ya kuleta maendeleo kwa jamii.
No comments