Dkt. Nchimbi: TAMISEMI puuzeni dosari ndogo ndogo za wagombea
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeiomba Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupuuza dosari ndogondogo ambazo zimejitokeza katika ujazaji fomu kwa wagombea wa vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Serikali za Mitaa.
Sababu za kutoa ombi hilo ni kutokana na mapingamizi mbalimbali yaliyotokana na makosa ya kisheria kwenye ujazaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo unaofanyika Novemba 27, 2024.
Makosa hayo yalisababisha wagombea hao kuenguliwa katika kinyang’anyilo cha uchaguzi huo.
Ombi hilo limetolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa Waziri mwenye dhamana, Mohamed Mchengerwa.
Balozi Dkt. Nchimbi aliyasema hayo wakati akisungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam.
“Kuna mapingamizi kwa vyama vyote yanayotokana na ukiukwa kwa Sheria katika kujaza fomu hizo, kwa sasa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uko katika kupitia rufaaa zilizotokana na mapingamizi ambayo yamesababishwa na makosa katika kujaza fomu.
“Wapo waliokosea kuandika herufi za majina, wengine katika nafasi inayotoka mgombea awe mwanamke lakini unakuta amejaza mwanaume, pia wapo waliokosea kujaza tarehe ya kuzaliwa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habaiBalozi Dkt. Nchimbi alisema kutokana na mapingamizi hayo, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya wagombea wa vyama mbalimbali kuwekewa mapingamizi ambayo yako sahihi kisheria.
“Kwa mujibu wa Sheria, kutokana na makosa hayo, waliokosea hawawezi kugombea hivyo tumekubaliana na Mwenyekiti, Wizara husika inayosimamia uchaguzi huu samehe makosa madogo madogo yaliyopo katika fomu ambazo zimewekewa mapingamizi.
“Tunajua Wizara inasimamia Sheria lakini kwa maslahi mapana ya Taifa letu ni vema wakasamehe ili wagombea wengi washiriki,” ameongeza.
"Tunajua makosa katika uchaguzi wa mwaka huu yako mengi lakini katika uchaguzi ujao yatapungua kwani tunaendelea kujifunza, demokrasia ya nchi yetu bado changa hivyo tuendelee kupeana nafasi.
“Waziri mwenye dhamana tunatambua Sheria zimefuatwa lakini demokrasia yetu ni change ambayo inaendelea kukua, uchaguzi huu makosa yatakuwa mengi lakini yataendelea kupungua,” amesema.
Amesema msimamo huo wa CCM una baraza zote za Rais Dkt. Samia hivyo ni vema ikaeleweka vizuri alizungumza na Mwenyekiti wetu wa Chama na ndio maana CCM imetoa msimamo huo.
Akijibu hoja ya wagombea wa CCM kupendelewa katika mchakato huo, Balozi Dkt. Nchimbi amesema hakuna pendeleo wa aina yoyote.
Amesema CCM imesimamisha wagombea katika nafasi zote zinazoshindaniwa, vyama vya upinzani vimeshindwa kusimamisha wagombea katika maeneo mengi.
No comments