Header Ads

ad

Breaking News

CCM Bagamoyo yapongeza Kitabu cha siasa za maji taka

Mwandishi wa kitabu cha Siasa za Maji Taka, Zainab Kihate

Na Omary Mngindo, Bagamoyo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kimempongeza Zainabu Kihate kwa maono yake ya kuandika kitabu alicholipatia jina la Siasa za Maji Taka.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa chama hicho Feisal Dauda, kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa kitabu kinachokosoa baadhi ya wanasiasa wanaotumia vibaya nafasi zao ndani ya tasnia hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dauda alisema kuwa mwandaaji wa kitabu hicho amekuwa na maono makubwa, huku akitolea mifano kadhaa ambayo imemkuta wakati akiwa katika harakati za kisiasa, hali ambayo alipambana nayo mpaka alipofikia sasa.

"Kitabu hiki kinaendana na ukweli ambao unaniumiza sana, tumeona Katibu wetu Iringa kapigwa risasi, hizo ndio tunazoziita ni siasa za maji taka, hata ukisimama ukawatukana wenzako zote ni siasa za majitaka," alisema Dauda.

Aidha, Katibu huyo amewaomba vijana waliomo katika siasa kutokukata tamaa na kwamba Taifa linawategemea "Kwa hiyo vijana wote mliomo kwenye mifumo ya siasa msikate tamaa, Taifa ili liende lazima tilisongeshe mbele," alisema Katibu huyo.

Naye Ibrahimu Gama alisema kuwa mwandishi wa kitabu hicho amefanyakazi kubwa sana, huku akieleza kuwa kuna wengi ambao wameandika vitabu lakini vimebaki kwenye mioyo yao au madaftari hawakutoa kwa jamii ili maarifa yao yaweze kupatikana.

"Kwakuwa leo umeingia kwenye rekodi tunakupongeza, umefanya jambo kubwa wenye kusoma wanasema ukitaka kuyaficha maarifa yaweke kwenye maandishi, kwakuwa umeweka humo watu wakisoma watayaelewa uliyokuwa umeyakusudia," alisema Gama.

Akizungumzia kitabu hicho, Kihate alisema kuwa ameguswa na wanasiasa wanaoitekeleza kwa kufuata Katiba na miongozo inayoiongoza, huku akisikitishwa na baadhi yao wanaoingiza chuki na ubinafsi.

Ibrahim Gama
Feisal Dauda (katikati), akiongoza na viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Siasa za Maji Taka
Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kitabu Siasa za Maji Taka

No comments