Simba yapunguzwa kasi na Toto African, zafungana 3-3
Simba, jana walizidi kupunguzwa kasi baada ya kutoka sare ya mabao 3-3, na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, anaripoti Daud Magesa, Mwanza.
Simba walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Felix Sunzu kwa kichwa, akiunganisha krosi iliyotoka kwa Juma Jabu dakika ya nane.
Lakini, bao hilo lilidumu dakika 11 tu, kwani Toto African ilisawazisha kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Darlington Enyiama, baada ya Obadia Mungusa kuunawa mpira ndani ya eneo la penalti.
Mohamed Soud aliipatia Toto African bao la pili dakika ya 34, kwa shuti lililomshibda kudakia kipa Juma Kaseja na kujaa wavuni, lakini Sunzu aliisawazishia Simba bao hilo dakika ya 59.
Toto wakicheza nyumbani huku wakishangiliwa na mashabiki wao, walifanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 60, lililofungwa na Idd Mobby.
Dakika ya 64, Simba walifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Patrick Mafisango na kuiwezesha timu yake kuondoka kanda ya ziwa ikiwa imejikusanyia pointi mbili, baada ya kulazishwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Kagaera Sugar wiki iliyopita.
No comments