Mzozo wa DRC: Mawaziri wa SADC na EAC wataka suluhu ya kudumu
![,](https://ichef.bbci.co.uk/ace/ws/640/cpsprodpb/vivo/live/images/2025/2/7/9ca27023-f109-41ba-bf72-82904c2f9da5.jpg.webp)
Na BBC
Mawaziri wa nchi za Jumuiya za maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki (EAC) wanataka suluhu ya kudumu kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mawaziri hao wamekutana leo mjini Dar Es Salaam, Tanzania katika kikao kinachotangulia mkutano wa marais wa jumuiya hizo utakaofanyika hapo kesho ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
“Hali ya usalama nchini DRC bado ni mbaya na inaathiri hali ya kibinadamu na kutishia usalama wa ukanda. Tunakutana sote hapa, tukiwa na mioyo ya kupata suluhu ya kudumu," amesema Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa mambo ya nje, Tanzania.
![.](https://ichef.bbci.co.uk/ace/ws/640/cpsprodpb/vivo/live/images/2025/2/7/9ed96a2f-a04c-498c-9ee0-c08c7787005d.jpg.webp)
Waziri wa masuala ya kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi ambaye ni mwenyekiti-mwenza wa mkutano huo amesema kuwa hii ni fursa mwafaka kwa EAC na SADC kuwasaidia watu wa DRC, akisema kwamba kuna haja ya kutekeleza kwa haraka mapendekezo ya mkutano wa marais.
“Hali hii inahitaji tuchukue hatua za haraka, kwa pamoja, na kwa njia endelevu," amesema Mudavadi.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wameuteka mji wa mashariki wa Goma, wamekuwa wakikabiliana vikali na majeshi ya serikali ya DRC.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibua watu 3,000 wamefariki kufuatia makabiliano baina ya M23 na wanajeshi wa serikali.
No comments