Header Ads

ad

Breaking News

Makocha wazawa, wachezaji wa kigeni kwangu safi - Karia

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akizungumza na wachezaji wa zamani kabla ya kuanza kwa bonanza lililoandaliwa na Kibada Veteran ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.Bonanza hili lilifanyika kwenye viwanja wa TFF Kigamboni.


Na Mwandishi wetu
RAIS wa Shirikisho la Mpira Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema si tu kwamba ana imani na benchi la ufundi la makocha wazawa, lakini pia analiamini na atalipa nguvu kwa mipango mikubwa ya soka la baadaye.

Akizungumza na wachezaji wa zamani ‘veterans’ waliokutana kwenye bonanza maalum lililoandaliwa na Kibada Veterans kwenye viwanja vya TFF Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, Karia alisema anaangalia kwa jicho la ziada mipango endelevu ya makocha wazawa na kwamba, wakiungwa mkono na kuaminiwa nchi itafika mbali kisoka.

Aliwaeleza wachezaji hao wa timu za Zanzibar All Star, Mandingo ya Tanga, Survey, makocha wa Kigamboni, Galactictico’s na waandaaji wa bonanza hilo, Kibada Veterans, kuwa fedha zilizopo kwenye soka la sasa ni tofauti na kipindi chao, hivyo walitazame pia kibiashara kwa kutokuwa wachoyo wa wachezaji wa kigeni.

" Mimi natetea sana uwepo wa wachezaji wa kigeni waliopo kwenye klabu zetu nchini, wanaipa biashara Azam Tv na Azam nao wanaleta pesa kwetu, pesa nyingi huingia kupitia Azam Max, kwa kuangalia ligi yetu, hiyo ni biashara ndugu zangu," alisema Karia.

“Hili huwapa changamoto ya kupambania namba vijana wetu, hivi sasa hatuziogopi klabu za kaskazini wala kusini, wachezaji wetu wamekomaa kwa kukutana hapahapa na wachezaji wakubwa wa kigeni, hili linatusaidia sana kiufundi, vijana wetu wana uzoefu wa kutosha.”

Alisema wachezaji na makocha wa kigeni wanalipa TFF, hivyo ni sehemu ya kipato ambacho husaidia hata timu za vijana zikaapo kambini. “ Tusijifungie kwenye maendeleo ya mpira miguu.”

Alielezea maendeleo ya kituo kikubwa cha michezo Kizimkazi, ukarabati wa Uwanja wa Amani, Benjamin Mkapa sanjari na viwanja vipya vya Dodoma na Arusha.

Mbali ya mipango ya timu zetu za taifa kucheza CHAN na AFCON, soka la wanawake, timu za vijana na soka la ufukweni, pia wachezaji hao walipata fursa ya kuelezwa awamu nyingine za mradi mkubwa ujenzi wa makao makuu ya TFF Kigamboni, ikiwemo majengo mapya, viwanja vitatu vipya mbali ya viwili vilivyopo, hospitali na majukwaa.

"Katika uongozi wangu nimewapa na ninaendelea kuwapa sana nafasi wachezaji wa zamani, akitolea mfano makocha wazawa waliopo Taifa Stars, soka la ufukweni, timu za vijana ambapo aliwaita mbele wachezaji wawili wa Kibada Veterans, Juma Kaseja na Mtwa Kihwelo ambao ni makocha wa timu za taifa za vijana na ufukweni.

“TFF tuna mpango mkakati wa kuvisaidia vyama vya mikoa ili viendane na kasi yetu ya maendeleo na kuwataka watanzania kujiandaa na mashindano ya CHAN na AFCON mwakani.”

Awali, Mwenyekiti wa Kibada Veterans, Benny Kisaka akimkaribisha Rais Karia, alisema timu hiyo ina malengo makubwa kwa wachezaji wastaafu na wana kibada kwa kujenga afya na maendeleo katika jamii iliyowazunguka.

" Kibada tumekusanya wastaafu wa ligi kuu, lakini hata wale waliocheza viwango vya kwenye vyuo na shuleni, lengo kuleta umoja na kuwa na afya njema miongoni mwa jamii iliyotuzunguka,"alisema Kisaka."

“Karibu Kibada Veterans Rais mwenye mafanikio katika soka la nchi hii, unatufanya watanzania tuione AFCON kama ya kawaida, tunaanza kuizoea, hongera sana kwa rekodi hii ya kipekee."

“Katika uongozi wako na hii si simulizi za mafanikio, kila mtu anaona kile unachokifanya katika utawala wako, hongera sana tunakupongeza hadharani maana umetenda hadharani, alisema Kisaka ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Miguu Dar es Salaam (DRFA).

Kibada Veterans ilitwaa ubingwa wa bonanza hilo la awamu ya kwanza kwa kuwafunga makocha wa Manispaa ya Kigamboni kwenye mchezo wa fainali mikwaju ya penalti 5-4. Zanzibar Old ilishika nafasi ya tatu wakati Mandingo kutoka Tanga ilishika nafasi ya nne.

No comments