CCM yasambaza viongozi na makada waandamizi nchi nzima
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuzindua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za CCM Mkoa wa Mwanza Novemba 20,2024, akiongoza viongozi na makada wa CCM waliotumwa maeneo mbalimbali nchini kwa kazi hiyo.
Balozi Nchimbi, ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Mwanza, atazindua kampeni hizo katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Uwanja wa Furahisha, Nyamagana jijini Mwanza.
Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ambao ni walezi wa mikoa mingine, pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), wamepewa jukumu la kuzindua kampeni hizo katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kwa tarehe hiyo hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Mongella atazindua kampeni mkoani Mbeya, wakati Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Mohamed Dimwa, akizindua kampeni Mkoa wa Katavi.
Viongozi wengine wa CCM waliopangiwa kuzindua kampeni ni pamoja na Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa NEC-Oganaizesheni, mkoani Geita.
Katibu wa NEC-Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla atazindua mkoani Dar es Salaam, huku Rabia Himid Abdalla ambaye ni Katibu wa NEC-Siasa na Uhusiano wa Kimataifa,atakuwa mkoani Kilimanjaro.
Wengine ni Dkt.Phillip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atazindua kampeni mkoani Dodoma, wakati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa atatikisa mkoani Kigoma.
Viongozi wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Abdulla Suleiman ambaye atazindua kampeni za mkoani Tanga, na Zuber Ali Maulidi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar atakuwa mkoani Singida.
Kwa uapnde wa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Taifa, Mary Chatanda atakuwa mkoani Arusha, wakati Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda atazindua kampenzi za mkoani Mtwara.
Viongozi wengine ni Halima Mamuya atakuwa mkoani Njombe, Nasir Ally Juma atazindua mkoani Tabora, Mohamed Aboud Mohamed ataamsha kampeni mkoani Iringa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM Taifa), Mohamed Ali Kawaida atazindua mkoani Morogoro.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania, Fadhili Maganya atakuwa mkoani Simiyu, Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko atajumuika na wanachama wa CCM Mkoa wa Mara na mwana CCM Hussein Bashe atatikisa mkoani Shinyanga.
Mwanachama Livingstone Lusinde atazindua kampeni za mkoani Manyara, Katibu wa Jumauiya ya Wazazi Tanzania Ally Hapi atakuwa mkoani Kagera, wakati Nape Nnauye ataanzisha safari ya kampeni mkoani Rukwa.
Wajumbe wengine ni Zainab Shomari atakayezindua kampeni z mkoani Lindi, Salim Abri (Asasi), atakuwa mkoani Ruvuma, Jokate Mwengelo atazindua kampeni za mkoani Pwani, Richard Kasesela ambaye ni Mjumbe wa NEC atakuwa mkoani Songwe.Mkakati huo wa kuzindua kampeni kwa mtindo wa ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wakuu na wanachama unaonesha jinsi CCM inavyothamini uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Pia, unadhihirisha dhamira ya kupata ushindi mkubwa dhidi ya vyama vya upinzani, ambavyo hadi sasa vimeshindwa kusimamisha wagombea wa kutosha kushindana kikamilifu.
No comments