Wahitimu Chuo cha Pasiansi watakiwa kuishi kwa maadili
WAHITIMU wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi wametakiwa kuyaishi maadili waliyofundishwa chuoni pindi watakapokuwa wakisubiri kuajiriwa, wakajiepushe na vitendo viovu na kamwe wasitumie mafunzo waliyopata wakiwa chuoni kinyume na sheria za nchi.
Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula, wakati akifunga mahafali ya 59 ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.
Mhe.Kitandula katika hotuba ya kuhitimisha mafunzo hayo aliishukuru taasisi ya Jane Goodall na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kufadhili mafunzo ya muda mfupi kwa vijana kutoka mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Pwani na Tanga.
Aidha, alitoa rai kwa wadau wa sekta binafsi zinazojishughulisha na uhifadhi wa wanyamapori au shughuli zinazoendana na uhifadhi wa wanyapori na utalii kutoa fursa mbalimbali kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali vinavyotoa mafunzo ya uhifadhi wa wanyamapori na misitu ili kuongeza tija na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Mhe.Kitandula alitoa wito kwa taasisi za serikali na binafsi kutumia huduma za ulinzi zinazotolewa Kampuni ya Ulinzi ya Pasiansi (Pasiansi Wildlife Security Company-PASCO), pale wanapokuwa wanahitaji huduma hiyo.
Kwa upande mwingine, Mhe.Kitandula ameipongeza Taasisi ya Taaluma wanyamapori Pasiansi kwa kutoa mchango katika sekta ya utalii kwa kutoa mafunzo ya uongozaji na usalama wa wageni, ambayo yanaendana na mkakati wa taifa wa kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025.
Katika mahafali ya 59 ya Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori vijana 70 wamehitimu astashahada ya usimamizi wa wanyamapori na himasheria, vijana 222 wamehitimu astahahada ya awali ya usimamizi wa wanyamapori na himasheria, vijana wanne wamehitimu astashahada ya waongoza wageni na usalama wa watalii na vijana 35 wamehitimu astashahada ya awali ya waongoza wageni na usalama wa watalii.
No comments