SERIKALI IMEPOKEA TAARIFA YA MWISHO YA UPEMBUZI YAKINIFU WA UJENZI WA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA-DTI, DODOMA
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Nicholaus Mkapa
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
Serikali imepokea taarifa ya mwisho ya upembuzi yakinifu wa ujenzi Chuo Mahiri cha TEHAMA (Digital Technology Institute - DTI) katika eneo la NALA, Dodoma kutoka kwa Mshauri elekezi kutoka Muungano wa Chuo Kikuu cha Hanyang kinachojumuisha Chuo Kikuu cha Hanyang, Kampuni za Uhandisi na Usanifu Majengo za Yooil Engineering & Architects, na Moon Engineering.Taarifa hiyo imepokelewa Septemba 5, 2024 katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kati ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Washauri Elekezi hao kutoka Korea Kusini.
Akiongoza Kikao hicho Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Nicholaus Mkapa amesema mradi huo unalenga kuimarisha mafunzo ya ujuzi na ubunifu katika TEHAMA, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini Tanzania.
“Serikali inatarajia kuwa uwepo wa chuo hiki utapunguza uhaba wa wataalamu wa TEHAMA, hasa katika teknolojia zinazochipukia (emerging technologies), na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utaalamu na uvumbuzi wa kidigitali kwa ukanda wa Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema Naibu Katibu Mkuu Mkapa.
Lengo la kikao hicho kilichofanyika tarehe 04 Septemba, 2024, lilikuwa ni kupokea na kujadili wasilisho la kukamilishwa kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA, na kufungua fursa ya kuendelea na hatua muhimu za kuanza kwa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho.
Uanzishwaji wa Chuo hicho cha kisasa ni matokeo ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuimarisha utaalamu na kuandaa wataalamu wa TEHAMA nchini, hususan katika teknolojia zinazoibukia (emerging technologies).
Ujenzi wa Chuo hicho pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo (2021-2026).
Akitoa wasilisho hilo lililojumuisha masuala muhimu yanayohusu elimu, mifumo ya TEHAMA, na usanifu wa majengo ya chuo, mbele ya uongozi wa Wizara, Meneja mradi wa mshauri elekezi huyo, Prof. Taejoon Park, ameshukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa ushirikiano mzuri katika kipindi chote cha upembuzi yakinifu na kuahidi kuendeleza ushirikiano kwa hatua zinazofuata.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo hicho wizarani, Mhandisi Dkt. Seleman Daudi Arthur amesema mradi huo utachangia kwa kiasi kikubwa katika uanzishwaji wa viwanda na ukuzaji wa ajira, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Dkt. Arthur amesema kukamilika kwa Ujenzi wa Chuo hicho Mahiri cha TEHAMA - DTI kutawezesha kuwa kitovu cha umahiri katika TEHAMA nchini, kikiwa na vifaa vya kisasa vya mafunzo na maabara za ubunifu katika maeneo ya teknolojia zinazoibukia, kama vile Roboti, Akili Mnemba (AI), Mtandao wa Vitu (IoT), Uchambuzi wa Takwimu (Data Analytics), na Usalama wa Mtandao.
No comments