Header Ads

ad

Breaking News

Mtandao wa barabara za wilaya wafikia kilomita 114,429.77 -Mtendaji Mkuu

Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, akizungumza  katika kikao kazi cha Wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Septemba 2,2024 jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR)


Na Mwandishi Wetu

WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), katika uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Haasan umetekeleza mambo makubwa kwa mafanikio hasa wa kuongeza mtandao wa barabara za wilaya kutoka kilomita 108,946.19 hadi kufikia kilomita 114,429.77.

TARURA imetangaza mafanikio hayo kwenye gazeti la Serikali Na.463 la Juni 25,2021,  kwamba Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020, iliielekeza serikali kuimarisha Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kwa kuongeza bajeti ili kukidhi mahitaji ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za mijini na vijijini.

 Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff,  katika kikao kazi cha wahariri na waandishi wa Habari na kusimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), leo Septemba 2,2024 jijini Dar es Salaam.

Seff amesema kuwa, mtandao wa barabara hizo umegawanywa katika makundi matatu, mtandao wa lami, changarawe na udongo, ambapo barabara za lami hadi kufikia Juni 2024 zilikuwa na urefu wa kilomita 3,337.66 sawa na asilimia 2.31.

Mhandisi Seff amesema kuwa, hali ya barabara hizo kilomita 2,743.81 zipo katika hali nzuri, kilomita 445.18 zipo katika hali ya wastani, wakati kilomita 148.68 zikiwa katika hali mbaya.

Kwa upande wa barabara za changarawe, jumla ya kilomita 42,059.17 ni sawa na asilimia 29.12, ambapo kilomita 21,890.53 zipo katika hali nzuri, wakati kilomita 15,792.23 zenyewe zina hali ya wastani na kilomita 4,426.41, zipo katika hali mbaya.

Afisa Habari Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiwakaribisha na kutoa neno la utangulizi kwa wahariri na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichofanyika Septemba 2,2024.

Mtendaji Mkuu huyo ameongeza kuwa, kwa upande wa barabara za udongo zenye kilomita 99,032.93 sawa na asilimia 68.57, ambapo kilomita 16,118.65 ziko katika hali nzuri, kilomita 34,739.20 hali yake ni ya wastani wakati kilomita 48,175.09 ziko katika hali mbaya. 

Kwa mtiririko huo unaonesha barabara nzuri, kwa pamoja ni kilomita 40,752.98, sawa na asilimia 28.22, wakati zenye hali ya wastani ni kilomita 50,926.60, ambazo sawa na asilimia 35.26, wakati zenye hali mbaya ni kilomita 52.750.18 ambazo ni sawa na asilimia 36.52.

"Kwasasa bajeti ya matengenezo ya barabara imeongezeka, miaka minne iliyopita ilikuwa shilingi bilioni 275, lakini kuanzia mwaka 2021/2022 imefikia shilingi bilioni 850, ni sawa na mara tatu ya bajeti ya zamani," amesema Mtendaji Mkuu wa TARURA, Seff.

TARURA imejiwekea malengo muhimu manne ya kusimamia ukarabati, ujenzi na matengenezo ya mtandao huo ambayo ni matengenezo ya miundombinu ya barabara ili kulinda uwekezaji uliofanyika, huku wakiendelea na matengenezo ya barabara na madaraja yatakapokamilika ili kuilinda miundombinu hiyo isiharibike.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Catherine Sungura, akiwashukuru wahariri na waandishi waliojitokeza katika kikao kazi

Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa, malengo yao mengine ni kuhakikisha wanaondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za wilaya ili zipitike wakati wote.

Kwa upande wa malighafi, Mhandisi Seff amesema TARURA wanatumia mali ghafi za ujenzi zinazopatikanan maeneo ya kazi  ambazo ni mawe, zinazochangia kupunguza muda wa ujenzi na husaidia kutunza mazingira.

Mhandisi Seff ameongeza kuwa, serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha barabara zinaboreshwa na kupitika wakati wote, huku zikijengwa nyingi kwa lengo la kuchochea maendeleo.

Kuhusu Bonde la Mto Msimbazi, amesema kaya 314 zinazoishi eneo hilo zimetambuliwa kuwa zitaathirika na uendelezaji wa bonde hilo pamoja na ujenzi wa daraja, hivyo mwezi huu watahakikisha wanaandaa daftari la fidia.

Mtendaji Mkuu huyo amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha wanakabiliana na mafuriko, hivyo eneo la chini la mto huo litaongezewa kina na kupanuliwa ili kuruhusu maji kwenda baharini kwa kasi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akitoa neno la shukrani katika kikao kazi hicho

Ameongeza kuwa, mradi huo ulianza kutekelezwa Februari 16, 2023, utatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ambazo ni dola za Marekani milioni 200, serikali ya Hispania itatoa euro milioni 30, na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi euro milioni 30.

Mhandisi Seff amesema katika mpango huo wa uendelezaji a bendo hilo, tayari asilimia 98 ya watu waliokuwa wakiathirika na mafuriko wamelipwa fidia na wameondoka.

Mtendaji Mkuu amesema TARURA huzipandisha hadhi  barabara za udongo kuwa za changarawe ama lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii.

Amesema mipango yao ya muda mrefu kitaifa na kimataifa, ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, manispaa na miji.

"Tathmini iliyofanyika mwaka 2022/23 ilibaini kuwa shilingi trilioni 1.635  zinahitajika kwa mwaka kuanzia mwaka 2023/24 ili asilimia 85 za mtandao wa Barabara za wilaya uweze kupitika misimu yote. Kwa sasa TARURA inapata wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwaka," amesema.



Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, akizungumza  katika kikao kazi cha Wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Septemba 2,2024 Jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR)

Watendaji wa TARURA wakifuatilia wasilisho la Mtendaji Mkuu Victor Seff
Wahariri wakiwa makini kusikiliza wasilisho lililotolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff

Wahariri wakifuatilia maelezo ya Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff

Wahariri wakisikiliza kwa makini wasilisho
Wahariri wakisikiliza

Wahariri wakiwa makini kusikiliza wasilisho




No comments