KAMATI YA BUNGE YAMTAKA MKANDARASI KUMALIZA UJENZI UWANJA WA NDEGE MIKUMI KWA WAKATI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imemwelekeza mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Kikoboga katika Hifadhi ya Taifa Mikumi, Badr East Africa Enterprises Ltd wenye gharama ya sh. bilioni 20.6 kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Ujenzi huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) ulianza Mei 12, 2023 na unatakiwa kukamilika Desemba 10, 2024.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ameyasema hayo leo Septemba 9,2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ya kukagua miradi ya REGROW kwenye hifadhi ya Taifa Mikumi, Mkoani Morogoro.
"Tunawapongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika na inaonekana lakini msisitizo wetu ni muda. Mkandarasi amalize kazi kwa muda uliopangwa" amesisitiza Mhe. Mnzava.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii , Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesikitishwa na kitendo cha kuchelewa kwa mradi huo huku akimtaka mkandarasi kukamilisha kwa wakati la sivyo sheria itachukua mkondo wake.
Ziara hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi na Watendaji na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Hifadhi ya Taifa Mikumi.
No comments