Bashe, Mpina wakutana jimboni Kisesa
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amefanya ziara kikazi jimboni Kisesa mkoani Simiyu na kukutana na Mbunge wa jimbo hilo, Luhaga Mpina ana kwa ana.
Bashe amemtaka mbunge huyo kuacha siasa katika zao la pamba, kwani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoogozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inahitaji kuona fedha zinazotengwa zinawanufaisha wakulima.
Waziri Bashe amewaahidi wananchi wa jimbo hilo kurejesha kitalu cha mbegu na kuwapatia ruzuku ya dawa za kuulia wadudu wanaoharibu zao la mahindi, pembejeo na mbegu za zao la pamba.
Mhe.Bashe akiwa jimboni humo na kufanya mkutano na wananchi wa jimbo hilo, alihudhuria ufungaji a mashindano ya michezo mbalimbali ya Mwandoya na kupokelewa na mamia ya wananchi.
Ametumia fursa hiyo kukutana na Mbunge Mpina, huku akimtaka kuacha siasa katika zao la pamba kwa maslahi ya wananchi na taifa.
“Rais Dkt.Samia amefanya kazi kubwa katika kilimo, Mhe. Mpina amesema hapa na mimi nasisitiza tuweke mambo mengine pembeni, aache siasa na sitaki siasa katika zao la pamba, nafahamu zipo changamoto lakini tulipotoka siyo tulipo, sitakubali mtu arudishe nyuma jitihada hizi, kwani wanaoteseka ni wananchi,”amesema.
Waziri wa Kilimo amekabidhi matrekta 40 jimboni humo na kuwataka maafisa kilimo na ugani kuacha kukaa mjini, badala yake waishi vijijini ili wawe na muda mzuri wa kuwasaidia wakulima kwa kutumia utaalamu wao na kufikia malengo ya serikali ya kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Bashe amewashukuru wazee wa kimila kwa kumsimika kuwa mtemi wa jimbo hilo, baada ya wazee hao kumsimika kuwa Mtemi (Chief) wa jimbo hilo.
“Nimesimikwa kuwa Mtemi wa Kisesa hivyo, Mpina akinitambia pale bungeni kwa kuingia na fimbo ya uchifu, nami nitaingia na yangu,”amesema Waziri Bashe.
Naye, Mkuu wa mkoa huo, Kennan Kihongosi amemhakikishia Waziri Bashe kuwa, yeye ndiye mwenye dhamana na mkoa huo, hivyo hawezi kuvumilia watu wanaotafuta umaarufu katika siasa kwa kuingiza masuala ya maendeleo.
“Nimetumwa kazi na Rais Dk. Samia, Simiyu ni ya kwanza ama ya pili katika kuzalisha pamba, ni zao la kiuchumi, hivyo sitaki wanasiasa watumie zao hilo kutafuta umaarufu. Shida zinazosemwa katika zao hilo si za kweli wananchi wa Kisesa msikubali kutumika,”amesema.
Naye, Mbunge wa jimbo hilo Luhaga Mpina ametumia fursa hiyo kumkaribisha Bashe Kisesa na kueleza kuwa, wana tofauti zao zilizowafika mahakamani, lakini yupo tayari kushirikiana naye katika masuala ya utendaji wa serikali.
"Nipo tayari kuweka tofauti zake na Bashe pembeni, tuungane katika masuala ya maendeleo na shughuli za serikali."
No comments