Wazanaki wazindua Biblia iliyotafsiriwa kilugha
KANISA Huru la Anglikana Dayosisi ya Tanzania, linatarajiwa kuzindua kitabu cha Biblia Takatifu kilichotafsiriwa kwa lugha ya kabila la Wazanaki.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk.Futakamba Mrisha ameiambia Jahmuri Digital kuwa uzinduzi huo utafanyika Agosti 2, mwaka huu kijijini Butiama ambapo mgeni rasmi anaratajiwa kuwa Chifu wa Wazanaki, Japhet Wanzagi.
Anasema Biblia hiyo itakuwa ya Agano Jipya lenye vitabu 29 na tayari nakala 10,000 zilizochapishwa nchini Korea Kusini zimewasili Tanzania.
Amesema alipata wazo la kuandaa kitabu hicho mwaka 2008 na mwaka 2009 alipata washirika
kutoka Shirika la Summer Instistute Linguste la nchini Marekani ambao waliunga mkono ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika.
Anasema kazi kubwa ya kutafasiri maandiko hayo limshirikisha Mchungaji wa Kanisa la Menonite Musoma,Sham Togoro.
“Kutokana na ushirikiano huu, mie na Mchungaji Togoro tulizunguka ‘nchi nane’ (maeneo) ambayo yanaunda eneo lote la Zanaki ambazo ukiangalia vizuri herufi zake zote zinaanza neno B,”anasema.
Ametaja maeneo hayo na watawala wake kwenye mabano kuwa Butiama (Nyerere Burito),Busegwe
(Ihunyo Tonge),Butuguri (Marwa Isasya),Buhemba Mabengu Wisariro, Bukabwa (Magero), Buruma (Magambo), Bumangi (Kyabwasi) na Buriga ya Mwanza (Manyori).
Anasema maeneo hayo ndiyo yanayounda Mahakamu Kuu ya Zanaki ‘Nyamuntenga’ ambayo inakuwa na wajumbe wawili sehemu husika.
Anasema kufika maeneo hayo kulikuwa na changamoto kubwa kutokana na uwapo wa pande mbili yaani Nyanza (magharibi) na Ruguru (mashariki), huku nia yao kubwa ikiwa ni kupata ukubalifu wahusika wa pande zote.
Anasema mwaka 2011 walizindua kitabu cha Injili ya Luka Mtakatifu na sasa wamerekodi mkanda wa simulizi ya maisha ya Yesu Kristo kwa lugha ya Kizanaki.
No comments