Header Ads

ad

Breaking News

WANYAMAPORI WANA MCHANGO MKUBWA KATIKA SEKTA YA UTALII



Na Beatus Maganja

WANYAMAPORI waliopo nchini wana mchango mkubwa katika Sekta ya utalii kwani huchangia zaidi asilimia 17 katika pato la Taifa.

 Akizungumza katika ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma Agosti 4,2024, Afisa Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Winniefrida Kweka alisema wanyamapori waliopo nchini wana mchango mkubwa katika pato Taifa, kwani huchangia zaidi ya asilimia 17.

 Winniefrida alitoa kauli hiyo wakati akitoa elimu ya uhifadhi kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma waliotembelea bustani ya wanyamapori hai iliyopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maonesho ya Nanenane mkoani humo.

 Alisema wanyamapori wanachangia sana kwenye sekta ya utalii kwa zaidi ya asilimia 17 za pato la nchi, asilimia zote hizo huchangiwa na utalii unaohusisha wanyama wa porini.

  Winniefrida alisema kutokana na faida zitokanazo na wanyamapori hao, TAWA inatumia maonesho ya Nanenane kuwaelimisha watanzania kuachana na mitazamo hasi kuwa, wanyamapori ni viumbe wasio na mchango chanya kwa Taifa.

 Mhifadhi huyo alisema kutokana na changamoto kutoka kwa baadhi ya wanyamapori wakali na waharibifu kama mamba, tembo, fisi na wengine, TAWA imekuwa ikielimisha umma juu ya mbinu rafiki za kuweza kuishi na wanyamapori hao na kuendelea kubaki salama kwa kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa nao.

 Ameweka wazi kuwa, chanzo kikubwa cha migongano kati ya wanyamapori hasa mamba na binadamu ni baada ya binadamu anapohitaji mahitaji yake sehemu ambayo wanyamapori hao wapo kama kwenye majini.

 Alisema kufuatia changamoto hiyo, Serikali kupitia taasisi zake za hifadhi imekuwa ikitoa elimu ya kujilinda dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na wanyama hao ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa vizimba vya mfano ili kuepusha madhara ya wanyamapori hao.

Winniefrida ametoa wito kwa wavuvi kufanya shughuli zao za uvuvi kwa njia zilizo sahihi na kuepuka kutega mitego ya samaki sehemu ambazo mamba wapo na kuachana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa, palipo na mamba ndipo samaki wapo wengi.

Maonesho ya mwaka huu yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na uvuvi" yalianza Agosti 1, 2024 na yanategemewa kufika kilele Agosti 8, 2024.




No comments