RC CHALAMILA AFUNGUA MAFUNZO YA UONGOZI MKOA WA DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewataka viongozi na watendaji mkoani humo kutumia mafunzo ya uongozi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi za kila siku ikiwemo kutumia fedha za Serikali vizuri katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye tija kwa wananchi na kuchagiza maendeleo nchini.
Chalamila ameyasema hayo Agosti 29, 2024 wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam yanayofanyika kwenye Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere ambapo amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha utendaji na kuimarisha mahusiano kati ya viongozi, watendaji na wananchi.
Amesema kupitia mafunzo hayo wanatarajia kuleta tija kubwa mojawapo kuongeza ufanisi wa kazi ambao utapelekea kuongeza mapato ya Mkoa lakini pia ,kutafsiri maono ya Mhe Rais kwenye kubuni miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji jijini humo.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ikiwemo wakuu wa wilaya za Mkoa wa Dar es salaam, mameya,wakurugenzi, wakuu wa idara na vitengo wamesema mafunzo hayo yataleta tija katika kuongeza uhusiano kati ya viongozi na wananchi pamoja na kuimarisha miradi ya maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila ameeleza matarajio ya Serikali kwa viongozi hao baada ya kumalizika mafunzo hayo ikiwemo ukuaji wa uchumi na kuimarika kwa mahusiano kazini.
Mkoa wa Dar es salaam umeanzisha utaratibu wa kuwajengea uwezo viongozi na watendaji ikiwa ni kuongeza tija kwenye ushirikishwaji wa makundi yote muhimu kwenye shughuli za maendeleo.
No comments