Header Ads

ad

Breaking News

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA, PSSSF, WCF WAINGIA UBIA KUMILIKI KIWANDA CHA CHAI CHA MPONJE

Msajili wa Hazina Bw.Nehemia Mchechu akizungumza wakati wa kutia saini umiliki wa Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichopo Korogwe mkoani Tanga, Agosti 9,2024

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

OFISI ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), wameingia ubia wa kumiliki Kiwanda cha Chai cha Mponde kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji, huku wadau mbalimbali wakitakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika zao la chai.

Katika ubia huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba Serikali inamiliki hisa asilimia 16, huku PSSSF na WCF wanamiliki asilimia 42 kila mmoja, jambo ambalo litaongeza kasi ya utendaji katika ushindani wa soko na kuifanya Taifa kupata gawio kama ilivyo kwa taasisi nyingine.

Akizungumza jijini Dodoma Agosti 9, 2024 katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya kumiliki kiwanda hicho iliyofanyika katika Ofisi ya PSSSF, Msajili wa Hazina Bw.Nehemia Mchechu, amesema uwekezaji huo utaongezeka thamani ya kiwanda kutoka shilingi milioni 790 zilizopo na kufikia bilioni 4.8.

Bw.Mchechu amesema wanatarajia kuwekeza shilingi bilioni nne ambapo hadi sasa tayari uwekezaji katika kiwanda hicho umefika bilioni 2.5.

“Kiwanda hiki kitafufua uchumi kwa wakazi wa Korogwe na wakulima wa zao la chai watapata soko la uhakika wa kuuza mazao yao,” amesema
Bw.Mchechu.

Ameongeza kuwa, kupitia uwekezaji huo, Serikali itanufaika na ulipaji wa kodi, huku akisisitiza umuhimu wa menejimenti kuongeza ufanisi katika utendaji ili waweze kutoa gawio kama ilivyo kwa taasisi nyingine.

“Nawashukuru sana PSSSF, WCF kwa kukubali wito wa kwenda kufanya uwekezaji katika sekta ya kilimo cha chai, ukiangalia tuna ardhi nzuri ambayo tunaweza kufanya uwekezaji kwenye  maeneo mbalimbali nchini,” amesema Mchechu.

aidha, amesema kuwa, Tanzania ina ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo inakubali kilimo cha chai hasa mikoa ya Iringa na Mbeya, huku akieleza kuwa kulikosekana wawekezaji wa viwanda katika zao la chai ambalo linalimwa kwa muda mrefu na kuleta tija.

“PSSSF na WCF wanapoonekana katika uwekezaji sekta ya kilimo itawavutia wadau wengine na kufanya vizuri sekta hii, kwani kwa muda mrefu wakulima walishindwa kulima zao la chai kutokana na kukosa soko la uhakika,” amesema Mchechu.

Mchechu amebainisha kuwa, Tanzania inazalisha kiwango kidogo cha chai na kufanya mauzo kuwa dola milioni 50 kwa mwaka, tofauti na  nchi jirani ya Kenya ambao wanauza  zaidi ya dola bilioni moja.

“Tupo chini katika mauzo kwa sababu tuna mwamko mdogo wa kufanya uwekezaji katika zao la chai, lakini leo tunashukuru tunawapa nafasi kiwanda hiki, menejimenti, bodi kuanza kukimbia katika utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Mchechu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema kuwa uwekezaji huo utaibua uchumi wa wananchi katika mkoa husika, kwani wakulima wengi wa eneo hilo watauza zao la chai katika kiwanda hicho.

“Ni busara imetumika kutumia fedha za Mifuko kuleta hapa kwa ajili ya kufanya uwekezaji na kuleta faida kwa kiwanda na wananchi,” amesema.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul -Razaq Badru amesema kuwa, uwekezaji huo ni sehemu ya mipango yao kutimiza jukumu linalotarajiwa na Serikali la kuwekeza katika maeneo yenye mchango kwa wananchi na wanachama wao.

“Tumefarijika kuwekeza katika sekta ya kilimo sehemu ambayo inatoa mchango mkubwa kwa Taifa, tutaendelea kushiriki katika maeneo mengine na kuleta tija kwa wananchi,” amesema.  (Green Waves Media)











No comments