Header Ads

ad

Breaking News

NGORONGORO YAAHIDI KUTENGA BAJETI YA ELIMU NA MIUNDOMBINU YA ANWANI ZA MAKAZI


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ngorongoro imeahidi kuanza kutenga bajeti sambamba na kuwashirikisha katika vikao, mikutano na shughuli nyinginezo Waratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) ngazi ya Wilaya ili kusaidia sekta zote kuona umuhimu wake.

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Bw. Thomas Nade wakati akijibu hoja zilizowasilishwa na Waratibu wa Anwani za Makazi Taifa na Wilaya waliofika ofisini kwake tarehe 26 Agosti, 2024 kutoa mrejesho wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi wilayani humo.


Bw. Nade ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ngorongoro, amesema kutokana na umuhimu wa elimu, miundombinu na mfumo wenyewe wa Anwani za Makazi, atahakikisha analifikisha kwenye vikao vya maamuzi ili katika robo ya pili ya mwaka wa fedha itengewe kiasi fulani.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo kimkoa, Mratibu wa Anwani za Makazi Taifa, Mhandisi Jampyon Mbugi amesema licha ya zoezi la uhakiki, usasishaji na usajili kwenda vizuri bado upo umuhimu mkubwa wa Idara za Kisekta kuwashirikisha waratibu wa NaPA kwa kuwa sasa ni zoezi endelevu.

Awali waratibu hao walitembelea Ofisi ya Mtendaji Kata ya Engurosambu Kijiji cha Engurosambu kukagua maendeleo ya Uhakiki ambapo changamoto iliyoainishwa na watendaji hao wa Kata, Kijiji na Mtaa ni upatikanaji wa mtandao na umbali wa boma moja hadi nyingine inayochangiwa na jiografia ya eneo hilo.

Naye Bw. Jasson Kalile, Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na ambaye anasimamia Kata mbili ikiwemo ya Engurosambu katika zoezi hilo, amesema hadi kufikia tarehe 26 Agosti zaidi ya asilimia 70 ya Anwani zilikuwa zimesasishwa.









No comments