Header Ads

ad

Breaking News

BALOZI KOMBO, CHUMI WATETA NA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi akisalimiana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman Visiwani Zanzabar Agosti 9,2024.


NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Mhe Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu wake Mhe. Cosato Chumi wamejitambulisha rasmi na kufanya mazungumzo ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, Ijumaa Agosti 9, 2024, Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Tukio hilo la kujitambulisha, baada ya mabadiliko ya hivi karibuni aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya Baraza la Mawaziri.

Akitoa salamu zake mbele ya ujumbe huo, Mhe.Othman amesema ni vyema kwa Taifa kutumia fursa zilizopo katika muunganiko wa Afrika Mashariki ili kujiimarisha kiuchumi.

Amesema, Afrika Mashariki siyo jumuiya tu, bali ni shirikisho la kufungua fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vyema, zitaleta tija kwa Taifa.

Aidha, amewaelekeza viongozi wanaosimamia Wizara hiyo, kuzitumia fursa zilizopo katika taasisi za kimataifa ili kuendana na kasi za kimaendeleo ulimwenguni.

"Zipo Taasisi kama WIPO, zinazobeba fursa nyingi ndani yake, ambazo mataifa ya Asia na Ulaya wanazitumia vilivyo kujinufaisha, lakini kwa Tanzania na Afrika bado tupo nyuma sana, tukizingatia hili ni jambo adhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu," amesema Mhe. Othman.

Mhe.Othman amewahimiza wahusika na watendaji wa Wizara hiyo kutoa elimu, kwa jamii za wazawa na hata wageni, juu ya mambo ya msingi yanayoihusu Serikali ya Muungano na Zanzibar ili kuondoa mkanganyiko, sambamba na kuwajengea uelewa mpana wananchi katika, kuelewa haki zao na maeneo sahihi ya kupata huduma kwa wakati.

Akieleza suala la tija kupitia sekta za utalii, kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Mheshimiwa Othman amehamasisha kuwepo kwa kumbi za mikutano zenye hadhi ya kimataifa ili kuvutia harakati za mataifa ya kigeni, kwa lengo pia la kulinufaisha Taifa.

Hivyo, Mheshimiwa Othman ameridhishwa na hatua ya ujumbe huo, kufika na kubadilishana mawazo, huku akiahidi ushirikiano mwema kwa maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri Mhe. Balozi Kombo ameahidi kwamba Wizara yake itafanya kazi kwa karibu na viongozi wakuu na watendaji wote waliopo Zanzibar ili kuleta ufanisi, na kuhakikisha wanayafikia malengo, kwa lengo la kuitangaza zaidi kimataifa.

Mhe. Kombo ambaye ameshika wadhifa huo hivi karibuni akitokea ubalozi wa Tanzania nchini Italia, ameahidi kuitendea kazi miongozo na mashauri yote aliyopewa, kwa Maslahi ya Taifa.

Viongozi wengine waliohudhuria Mhe. Denis Lazaro; Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji; pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ilyasa Juma Pakacha.


No comments