Header Ads

ad

Breaking News

ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 16.9 ZATUMIKA KUIMARISHA MAWASILIANO KANDA YA ZIWA




Picha mbalimbali wakati Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye na Mbunge wa Jimbo la Ushetu (CCM), Mhe. Emmanuel Charahani (aliyepanda Mnarani) wakati wa kukagua ujenzi wa mnara uliojengwa na Kampuni ya Honora kijiji cha Ngokolo Kata ya Bukomela ambao ni miongoni mwa minara 7 inayojengwa Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kabla ya kuhitimisha ziara yake katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa.



Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Shinyanga

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb), amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imetoa zaidi ya Shilingi Bil 16.89 kwa mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa ili kujenga minara ya mawasiliano.

Waziri Nape amesema, fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa minara 117 katika kata 113, vijiji 240 vya mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga.

Amebainisha hayo Julai 19, 2024, wakati akiwahutubia wananchi katika Kata ya Bukomela, Wilaya ya Kahama, Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, alipokuwa akitoa majumuisho ya ziara yake ya siku tano katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Ndugu zangu wa Ngokolo, ndani ya huu Mradi wa Tanzania ya Kidigitali, upo mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa minara 758, tunapeleka mikoa 26 ya Tanzania Bara na ndiyo maana napita mkoa kwa mkoa, na minara hii tumelenga kuwaunganisha Watanzania milioni 8.5 na wote tunataka waguswe na huduma za mawasiliano kama vile Ngokolo na maeneo mengine yalivyounganishwa, na haya ndiyo maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Nape na kuongeza;

“Katika mikoa niliyopita ukiwemo huu wa Shinyanga, katika mradi wa bilioni 200 na kitu za ujenzi wa minara Tanzania nzima, fedha hizo zitatumika kupeleka hiyo minara kwenye maeneo ya vijijini, na katika mikoa mitano niliyopita bilioni 16.89 zimeletwa kuhakikisha hakuna Mtanzania anaachwa nje ya huduma za mawasiliano,”

Amesema, katika mikoa hiyo mitano, Serikali imekusudia kuwafikia Watanzania 1,868,996, wakiwemo wa Kishapu ambako minara saba inajengwa ukiwemo huo wa Ngokolo uliojengwa na Kampuni ya Honora (zamani Tigo).

Waziri Nape ameipongeza kampuni hiyo ya Honora kwa kujenga mnara wenye uwezo mkubwa wa 2G, 3G na 4G uliopita malengo kwa kuvifikia vijiji vitano tofauti na malengo ya awali ya kufikia vijiji viwili huku wanufaika wakiwa ni watu 20,000.

Akikagua ujenzi wa mnara uliojengwa na Kampuni ya Halotel ambao Serikali imetoa ruzuku ya s
hilingi milioni 145, Waziri Nape amesema, wakazi 12,100 wa vijiji vinne vya Busangwa, Mwanima, Mwajipugira na Pambe wilayani Kishapu watapata mawasiliano.




















No comments