Header Ads

ad

Breaking News

Watoto 300 wafaidika na matibabu ya moyo kupitia CRDB Marathon


Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akikabidhi bendera za nchi za Tanzania, Burundi na Congo kuashiria uzinduzi wa mbio za CRDB msimu wa tano zitakazofanyika katika nchi hizo mwezi wa nane mwaka huu kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI, matibabu ya akina mama wajawazito wenye mimba hatarishi na fistula pamoja na kuwezesha vijana kwa kuwajengea uwezo katika nyanja mbalimbali.


 Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

Watoto zaidi ya 300 wamefanyiwa upasuaji wa moyo kutokana na fedha zilizopatikana katika misimu minne ya mbio za CRDB Marathon tangu mwaka 2020 hadi 2023.

Mbio hizo zinazofanyika kila mwaka mwezi Agosti zimekuwa zikijikita katika kusambaza tabasamu na kuboresha afya na mazingira kutokana na sekta hizo kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio za CRDB benki msimu wa tano, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema mbio hizo zimekuwa zikichangia jitihada kubwa inayofanywa na Serikali.

“Kama benki tunaamini tunaweza kurejesha tabasamu, kuleta tumaini jipya kwa jamii na kuboresha nguvu kazi ya taifa,” alisema Abdulmajid.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge aliushukuru uongozi wa CRDB kwa kuwathamini watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI kwa kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto hao.

Dkt. Kisenge alisema CRDB imekuwa mdhamini mkubwa wa kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo kwa miaka minne mfululizo hivyo kujenga uhusiano mzuri na Taasisi hiyo.

“Tunawashukuru sana benki ya CRDB kwa kurejesha tabasamu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI kwani matibabu ya moyo ni ya gharama na watoto wengi wanatoka kwenye familia ambazo kwa namna moja hawana uwezo wa kugharamaia matibabu hayo,” alisema Dkt. Kisenge

Naye, Mkurugenzi Mtendaji CRDB Foundation Tully Mwambapa alisema mbio za CRDB msimu wa tano zimedhamiria kuwaleta watu wa ndani na nje ya nchi pamoja, kupanua wigo wa uwekezaji katika jamii pamoja na kuboresha maisha yawatu hasa wale wanaohitaji huduma za afya.

 “Mbio za CRDB benki msimu wa tano zitaanzia nchini kongo Agosti 4, kufuatia nchini Burundi tarehe 11 Agosti, na kumalizia nchini Tanzani  Agosti 18, mwaka huu,” alisema Tully.

Tully alisema upande wa Tanzania fedha zitakazopatikana CRDB itaendelea kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto wenye uhitaji, matibabu ya kina mama wajawazito wenye mimba hatarishi na fistula pamoja na kuwezesha vijana kwa kuwajengea uwezo katika nyanja mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, viongozi wengine pamoja na watoto waliofanyiwa upasuaji wa moyo kupitia fedha za CRDB benki marathon wakati wa ufunguzi wa mbio hizo msimu wa tano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Watoto waliofanyiwa upasuaji wa moyo kupitia fedha za CRDB benki marathon wakitambulishwa wakati wa ufunguzi wa mbio CRDB benki Marathon msimu wa tano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi wakifuatilia hutuba zilizokuwa zikitolewa wakati wa ufunguzi wa mbio za CRDB benki marathon msimu wa tano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam
Viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi wakifuatilia hutuba zilizokuwa zikitolewa wakati wa ufunguzi wa mbio za CRDB benki marathon msimu wa tano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Picha zote na JKCI

No comments