Header Ads

ad

Breaking News

Wananchi wahimizwa kutumia Mifumo iliyowekezwa na Serikali


Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, amewataka watanzania kuendelea kujibidisha kutembelea mifumo mahsusu iliyowekezwa na Serikali ili kuijua mitaa na Postikodi kwa ajili ya kuzifahamu Anwani zao za Makazi. 

Amewataka pia wananchi wanaotembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa, kutembelea banda la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kupata elimu kuhusu mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kwa kuwa una faida nyingi ikiwemo huduma ya kupata barua ya Utambulisho kidijitali.

Dkt. Yonazi ametoa wito huo leo tarehe 04 Julai, 2024 wakati alipotembelea Banda la maonesho la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kujionea huduma zinazotolewa na wizara hiyo kwa wananchi katika maonesho hayo.

"Serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo ya utambuzi. Hapa tunayo pia huduma ya Barua za Utambulisho kutoka katika Serikali za Mitaa, ni huduma nzuri sana inarahisisha, inampa mwananchi utambulisho sahihi" amesisitiza Dkt Yonazi.

Amesema kuwa ni matumaini yake kwamba wananchi wakiielewa vema huduma hii watapata barua zao bila usumbufu na hivyo kusaidia katika kuchangia Uchumi wa Kidigitali.

 Akitoa maelezo ya namna mfumo huo wa Anwani za Makazi unavyofanya kazi mmoja wa Maafisa kutoka Wizara hiyo Bi. Rehema Chillo amesema vitu vya msingi vinavyohitajika ili kuhakiki Anwani yake ya makazi ni kuwa na namba ya simu, Namba ya kitambukisho cha Taifa (NIDA) au Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN).




No comments