Header Ads

ad

Breaking News

WANANCHI RUFIJI WAISHUKURU TAWA KWA KUCHEPUSHA MTO

Salum Kassim Njenge mkazi wa Kijiji cha Ngarambe wilayani Rufiji mkoani Pwani akiishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kwa kuuchepusha mto uliobadili uelekeo na kusababisha athari kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho.


Na. Beatus Maganja

Wananchi wa Kijiji cha Ngarambe, Kata ya Ngarambe Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani wameishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),  kwa msaada wa kuchepusha mto uliobadili uelekeo wake kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu zikiambatana na kimbunga HIDAYA na kusababisha kuelekea katika makazi na mashamba ya wananchi  na kusababisha uharibifu mkubwa.

Wananchi hao wametoa shukrani hizo Julai 26, 2024 kwa TAWA kupitia uongozi wa Pori la Akiba Selous Kituo cha Kingupira kwa kutoa mashine inayosaidia kuchepusha mto huo kutoka makazi ya watu, jambo ambalo wamekiri kuwa litasaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao.

Salum Kassim ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ngarambe amesema mvua kubwa zilizonyesha mwaka huu ambazo ziliambatana na kimbunga HIDAYA zilisababisha athari kubwa kwa wakazi wa Kijiji hicho kama vile kuharibu makazi yao kwa kubomoa nyumba, kuharibu majengo ya shule na vyoo vya shule hasa baada ya Mto kubadili uelekeo wake kutokana na kujaa maji mengi.

Salum anasema kutokana na ushirikiano mzuri na ujirani mwema baina ya Kijiji hicho na Pori la Akiba Selous , waliomba msaada TAWA kupitia uongozi wa Kituo cha Kingupira kilichopo katika Hifadhi hiyo na uongozi huo kukubali kutoa mashine ambayo inaendelea kufanya kazi ya kuchepusha mto ili kuokoa maisha na mali za wananchi hao.

Kaimu Kamanda wa Pori la Akiba Selous ambaye pia ni msimamizi wa Kitengo cha ujirani mwema, Jimmy Mshana amesema Kijiji cha Ngarambe ni majirani wa Hifadhi hiyo ambao wamekuwa na ushirikiano nao wa muda mrefu katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuhifadhi hivyo baada ya kuona wamepata changamoto hiyo walilazimika kutoa msaada wa haraka ili kuweza kuwaokoa kwa kuchepusha mtu huo ili wasije wakapatwa madhara makubwa zaidi.

Amesema kazi ya kuchepusha mto huo imefanyika kwa ushirikiano mkubwa kupitia viongozi mbalimbali wa kata na kijiji husika pamoja na wananchi wote kwa ujumla.

TAWA imekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi waishio pembezoni mwa Hifadhi mbalimbali inazozisimamia nchini kupitia progamu za ujirani mwema jambo ambalo limewafanya wananchi hao wajivunie uwepo wa Taasisi hiyo katika maeneo yao.

Ikumbukwe kuwa mapema ,waka huu TAWA ilitoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula na magodoro kwa wananchi wa Wilaya ya Rufiji waliopatwa na mafuriko pamoja kuwapa elimu ya namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko.
Said Mbagae Muba Mkazi wa Kijiji cha Ngarambe wilayani Rufiji mkoani Pwani akielezea athari za mto uliochepuka kwenye njia yake
Kaimu Kamanda wa Pori la Akiba Selous ambaye pia ni msimamizi wa Kitengo cha ujirani mwema, Jimmy Mshana  akielezea uchepushaji mto uliosababisha athari katika Kijiji cha Ngarambe wilayani Rufiji mkoani Pwani

No comments