Header Ads

ad

Breaking News

WAGOMBEA URAIS TLS WATAJA MIKAKATI YA KUWAINUA MAWAKILI WACHANGA

Wagombea wa nafasi ya Urais katika Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) wakiwa kwenye mdahalo. 


Na Mwandishi Wetu

WAKATI uchaguzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), ukitarajiwa kufanyika Agosti 2,2024 jijini Dodoma, wagombea nafasi ya urais wamejinadi namna ya kujenga chama hicho kwenye misingi yenye nguvu ikiwamo kuondokana na vishoka katika taaluma hiyo.

Wagombea wanaowania nafasi hiyo ni Wakili Sweetbert Nkuba, Paul Kaunda, Revocatus Kuuli, Emmanuel Muga, Ibrahim Bendera na Boniface Mwabukusi.

Akizungumza juzi kwenye mdahalo wa wagombea hao jijini Dar es salaam, Mgombea wa Urais TLS, Wakili Revocatus Kuuli, alisema “Wako Mawakili vishoka ambao ni matapeli tu na kwanza huwezi kuwaita Mawakili. Matapeli wa kisheria hawatakuwepo nikiwa Rais wa TLS.”

Alisema kuwa Wakili kishoka ni kosa la jinai na vyombo vinavyoshughulika na jinai kama polisi vina wajibu wa kushughulika na watu hao.

“Kuna baadhi ya watu wanakiona chama hicho kupoteza ubora, lakini wagombea ambao tunagombea sasa tumeweka mikakati ya kukirudisha chama kuwa na nguvu na kutekeleza misingi iliyowekwa ya chama,”alisema.

Mgombea Wakili Boniface Mwabukusi alisema atarudisha taaluma ya uwakili katika misingi kwa kuwa TLS ni taasisi kongwe.

“Mimi ni simba nitakayeongoza kundi la simba na watanzania wataanza kuona uwepo wa chama hiki kwa kuwa TLS ina wajibu kwa wananchi, serikali, wanachama na utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka katika mhimili ya dola,”alisema.

Alisema TLS ndio kiungo wa kuifanya nchi ishamiri kiuchumi, kisiasa na kidemokrasia.

“Nataka kuleta umoja kwenye uwakili kwasasa umegawanyika, tunapokuwa na TLS yenye kuwajibika nchi zinavamiwa kiuchumi ni wajibu wa TLS kuongoza watanzania kujua ukweli wa kisheria wa mikataba ya kimataifa na sera tunazoingia, nikipewa nafasi anakwenda kubadili mfumo wa watu kufikiri TLS ni jukwaa la kutafuta mambo fulani.”

“Hatutaruhusu mawakili kunyanyasika katika taifa hili, kanuni zinazoongoza malipo kwa mawakili zinakatisha tamaa, tusipokuwa na ulinzi katika taaluma yetu hakuna aliye salama,”alisema.

Mgombea Wakili Emmanuel Muga, alisema akichaguliwa ataimarisha utawala kwa kutengeneza kamati zenye uwezo wa kufanya kazi na kuifanya TLS kufuata taratibu za kisheria na sio kuendesha mambo yake kiholela.

“Nitasimamia wajibu wa TLS kwa wanachama, serikali na kwa wananchi, na mimi sitakuwa Rais wa TLS wa kufoka foka kwa kuwa sina mamlaka yangu peke yangu ya kutoa tamko ambalo halijatokana na kamati ya uongozi wa TLS,”anasema.

Naye, Mgombea Wakili Sweetbert Nkuba alisema kama atachaguliwa kuwa Rais wa TLS atahakikisha taasisi hiyo inalinda heshima yake na kuwasambaratisha vishoka walioko kwenye kada hiyo ambao hawajasomea sheria.

Alisema atahakikisha mawakili wote wanasajiliwa na ofisi zao zitambulike kisheria ili kuwabaini mawakili wababaishaji.

“Nitaimarisha TLS tunatakiwa kuwa na nguvu na sauti moja ambayo itasaidia uimara wa chama, hivyo ni muhimu kupata viongozi makini wenye dhamira thabiti ya kusimamia chama na si ujanja ujanja,”alisema.

MAWAKILI VIJANA

Wakili Nkuba alisema akipata nafasi hiyo atahakikisha mawakili vijana chipukizi hawatozwi ada nyingi kuwa mawakili, kuwajengea weledi kwa kuwa wengi wao wanashindwa kufanya kazi zao kwa kukosa mitaji na maeneo ya kufanyia kazi.

Aidha, Mgombea Wakili Paul Kaunda alisema anataka kuwalinda na kuwatetea mawakili wachanga kwa kuwaongezea thamani na heshima ikiwamo kuanzisha Wakili APP ambayo watajisajili na itarahisisha wao kupata wateja.

Mgombea Wakili Ibrahim Bendera alisema amedhamiria kuwaunganisha mawakili vijana na wale wenye uzoefu ili kuwasaidia kujijenga kitaaluma kutokana na wengi wao kushindwa kuanzisha ofisi zao kwa kukosa mitaji huku Wakili Muga akisema ataanzisha utaratibu wa kuwasaidia mawakili wachanga kwa kusimamiwa na mawakili wazoefu.  (Green Waves Media)

No comments