Header Ads

ad

Breaking News

Vifungashio vya madini kuboreshwa kudhibiti utoroshaji

Na Vicky Kimaro, Tume ya Madini

TUME ya madini ipo kwenye mchakato wa kuboresha vifungashio vya madini katika masoko ya madini nchi nzima ikiwa ni mkakati wa kuendelea kudhibiti utoroshaji wa madini.

Hayo yamesemwa na Aloyce Bwana Mteknolojia Maabara katika Maonesho ya 48 Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba).

Amesema, mkakati wa Tume kuanzia mwaka huu wa fedha 2024/2025 ni kuhakikisha vifungashio katika masoko yote ya madini vinakuwa vya aina moja tofauti na ilivyo sasa vinatofautiana.

Amesema, kuwa na aina moja ya vifungashio itapunguza utoroshaji wa madini unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu na kuinyima Serikali mapato.

“Kuwa na vifungashio vya aina moja itasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini, masoko ya madini yamesaidia kupunguza utoroshaji wa madini kwa kiasi kikubwa lakini kama Tume ya Madini tutaendelea kuchukua hatua madhubuti kudhibiti zaidi utoroshaji wa madini, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi,”amesema.

Naye, Baiton Mtebe Mjiolojia akizungumzia masoko ya madini amesema masoko yalianzishwa kama njia mojawapo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika la madini yao baada ya kuchimba, Serikali kupata mapato na takwimu sahihi za madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo wa madini, kuuza madini kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume ya Madini kulingana na soko la dunia. Vilevile kudhibiti utoroshaji wa madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Amesema mpaka sasa Tume ya Madini ina masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 102 nchini ambayo yameongeza mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye mapato kutoka asilimia tano hadi asilimia 40 Mwaka 2022/2023.

Amesisitiza kuwa masoko ya madini yamepunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya utoroshaji wa madini pamoja na kuleta ushindani kwa wafanyabiashara wa madini kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini.




No comments