Header Ads

ad

Breaking News

Uwekezaji Bandari Dar waduwaza viongozi UVCCM

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), Bw. Mohamed Kawaida, akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuhitimisha ziara yake na viongozi wakuu wa umoja huo walioambatana wenyeviti na makatibu wa mikoa yote ya Tanzania Bara walipotembelea Bandari ya Dar es salaam kujionea na kujifunza, ambapo wameshangazwa na uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vifaa bandarini hapo jana.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetembelea maeneo ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam uliofanywa na kampuni ya DP World na kusema uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ufanisi mkubwa bandarini hapo kwa maendeleo na ustawi wa nchi.

Akizungumza baada ya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM , Bw. Mohamed Kawaida ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kizalendo wa kuruhusu uwekezaji huo ambao una manufaa makubwa kwa taifa.

Amesema ripoti ya utendaji iliyowasilishwa na uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), umeonesha kuongezeka kwa ufanisi na kazi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo bandarini hapo, tofauti na hofu iliyokuwepo hapo awali ya watu waliokuwa wakipinga uwekezaji huo.

“Tukiwa kama wasimamizi wa Serikali katika utekelezaji wa ilani ya CCM, tumeamua kutembelea Bandari ya Dar es Salaam kujionea shughuli mbalimbali zinavyofanyika, tumefurahishwa na ufanisi wake baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika,” amesema Kawaida.

Amesema lengo kubwa la ziara hiyo ambayo pia ilihusisha wenyeviti na makatibu wa Umoja wa Vijana kutoka mikoa yote nchini, lilikuwa kujionea na kujifunza namna kazi zinavyofanyika bandarini hapo.

“Mimi na viongozi wenzangu wote wa UVCCM tumefurahishwa na tija ya uwekezaji huu katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema na kuongeza kuwa,  hapo awali kulikuwa na maneno mengi ya upotoshaji kwamba, uwekezaji huu hauna tija kwa taifa na watanzania wengi wangepoteza ajira na wafanyabiashara kukimbilia bandari nyingine za nchi jirani.

Alisema mwekezaji DP World amewekeza fedha nyingi katika miundombinu na vitendea kazi uliochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa shehena za mizigo katika bandarini,” alisema na kuipongeza pia menejimenti ya TPA.

“Lakini katika ziara hii tumejionea hali tofauti kabisa, ambapo ufanisi na upakuaji mizigo umeongezeka baada ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vitendea kazi kufanyika,” amesema kiongozi huyo akiwa ameongozana na Kamati ya Utekelezaji ya chama hicho katika ziara hiyo.

“Hii inamaanisha kuwa, mapato yanayotokana na uwekezaji huu yameongezeka na kuwa na tija katika maendeleo ya nchi yetu,”amesema Kawaida na kuongeza kuwa, Tanzania imebarikiwa neema ya kuwa na bandari hii inayohudumia nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji na Zambia.

Alisema uwekezaji kama huo ulihitajika ili kuendeleza kukuza soka la biashara katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Dhana ya nchi yetu ni kuingiza kipato kwa maendeleo ya nchi kupitia maboresho ya sekta ya usafirishaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya reli ya SGR ambayo pia tumeitembelea na kuridhishwa na maendeleo yake,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi ya Mkurugenzi wa TPA, Bw. Plasduce Mbosaa, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw Mrisho Selemani Mrisho amesema kuwa, viongozi wa umoja huo wamefurahishwa na ufanisi unaofanywa na mwekezaji DP World bandarini hapo kama ilivyotarajiwa na kujifunza mengi wakati wa ziara hiyo.

Amesema ili kuleta ufanisi na tija, mwekezaji DP World ameweka vitendea kazi mbalimbali bandarini hapo katika kuhudumia shehena za mizigo bandarini na kufanya ufufuaji wa mashine (SSG), ambazo awali zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi kwa sababu ya matatizo ya umeme, lakini sasa hivi mwekezaji anazalisha umeme kupitia mashine hizo.

Lakini pia mwekezaji ameweka mashine za kuhudumia makasha katika uboreshaji wa miundombinu hiyo.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuitumia bandari hiyo kutokana na mageuzi makubwa yanayofanyika katika kuharakisha kazi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini hapo.

Ripoti ya utendaji kazi wa bandari hiyo iliyowasilishwa wakati wa ziara hiyo kwa viongozi wa umoja huo imeonesha mafanikio makubwa yamepatikana baada ya Serikali chini ya Rais Samia kuridhia uwekezaji wa DP World bandarini hapo.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2020/21/22/2023), mapato ya Bandari ya Dar es Salaam yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 27.2 kwa mwaka, kutoka kiasi cha shilingi bilioni 801.7 hadi trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kulikotokana na kuongezeka kwa shehena zikiwemo kutoka nchi za jirani.

Lakini pia ripoti hiyo imeonesha kuongezeka kwa idadi ya meli kwa wastani wa asilimia 7.5 kwa mwaka, ambapo mwaka 2021/2022 meli 1,569 zilitia nanga bandarini hapo na mwaka 2022/2023 zilikuwa meli 1,743.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Mrisho Seleman Mrisho akisisistiza jambo kwa ujumbe wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM) wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Bandari hiyo jana.
Viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wakitembelea bandari ya Dar es Salaam jana, ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Taifa Bw. Mohamed Kawaida.

No comments