Header Ads

ad

Breaking News

The Reds yasaidia yatima Morogoro

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kusherehekea siku ya Klabu ya Simba Agosti 3,2024, Kundi Sogozi la The Reds Community ambalo linahusisha wanachama na washabiki wa timu hiyo kimetembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa Kituo cha Watoto yatima cha Raya kilichopo Lugono mkoani Morogoro.

Msaada huo wa wana Simba umewasilishwa leo na Mwenyekiti wa The Reds Community, Zahran Rashidi akiwa ameambatana na wana kundi kwa niaba ya kundi hilo ambalo limedhamiria kuonuana kiuchumi na kijamii.

Mwenyekiti huyo amesema kundi la The Reds Community limeanzishwa na wana Simba kutoka pande zote za nchi na nje ya nchi kwa lengo la kusaidiana, hivyo katika kuelekea siku ya Simba wameamua kuchangishana fedha ambazo zimenunua mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kusaidia watoto yatima 90 wa Kituo cha Raya.

"Sisi The Reds Community tunaamini jamii ni muhimu na kwa kuthibitisha hilo tumeweza kuchanga takribani Shilingi miloni 1.5 ambazo zimetumika kusaidia watoto 90 yatima, niwashukuru sana wana kundi ambao wamejitolea.

Zahran amesema michezo ni moja ya eneo ambalo linahusisha watu wengi, hivyo msaada waliotoa unaonesha namna michezo inayounganisha jamii.

"Tumekabidhi kwenye Kituo cha Raya, mchele kilo 90, ngano kilo 25, sukari kilo 50, sembe kilo 50, chumvi karibu moja, sabuni ya unga viroba vitatu, maharage kilo 25, mafuta ya kula lita 20, madaftari, taulo za kike, kalamu, pipi na vingine," amesema.

Mwenyekiti huyo amesema dhamira ya kundi lao ni kuhakikisha linasaidia jamii yenye uhitaji kila inapopata fedha za kufanya hivyo.

Mlezi wa kituo hicho, Madam Raya ameishukuru The Reds Cimmunity kwa moyo waliounesha na amewakaribisha tena kusaidia watoto hao ambao wanauhitaji mkubwa.

Amesema kituo hicho chenye watoto yatima 90 kwa sasa watoto 22 wanasoma elimu ya sekondari huku watoto 50 wakisoma shule ya msingi.

Watoto hao walipata muda wa kuomba dua ya pamoja na wawakilishi wa The Reds Community na wameitakia mafanikio ya Timu ya Simba katika msimu wa 2024/25.











No comments