Header Ads

ad

Breaking News

Ridhiwani Kikwete akabidhi madawati 500 jimboni Chalinze

Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri wa Utumishi, Ridhiwani Kikwete akisalimiana na wanafunzi katika shule mpya iliyopewa jina la Ridhiwani Kikwete, wakati wa hafla ya kukabidhi madawati hayo. Picha zote na Omary Mngindo.

Na Omary Mngindo, Bwilingu

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete (Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora), mwishoni mwa wiki amekabidhi madawati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 37.5 kupitia mfuko wa jimbo.


Madawati hayo yanayogawanywa katika shule mbalimbali lengo kuboresha upatikanaji wa elimu bora ndani ya jimbo hilo, huku kukiwa na mipango zaidi ya kuongezwa kwa madawati kwenye shule nyingine.

Hayo yameelezwa na Ridhiwani wakati akikabidhi madawati hayo katika Shule ya Ridhiwani Kikwete, iliyopo Bwilingu ikishuhudiwa na Mkurugenzi Ramadhani Possi, Mwenyekiti wa Halmashauri Hassani Mwinyikondo, Diwani Nassa Karama na viongozi mbalimbali.

"Najisikia vibaya kuona wanafunzi wanakaa chini, rais wetu Dkt. Samia Suluhu anafanyakazi nzuri katika sekta zote, nitahakikisha shule zetu zinazidi kuboreshwa ili watoto wetu waendelee kupata elimu bora zaidi," alisema Ridhiwani.

Mwenyekiti wa halmashauri Mwinyikondo alimwambia Naibu Waziri kwamba halmashauri itaongeza madawati mengine, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za mbunge wao, na kwamba Chalinze haina shida ya fedha.

"Kwanza nikupongeze mbunge wetu, kazi kubwa tunaiona katika jimbo letu, pia unamsaidia Rais wetu Mama Samia katika nafasi yako ya Naibu Waziri wa Utumishi, katika ili tunakuunga mkono kwa kuongeza madawati zaidi," alisema Mwinyikondo.

Diwani Nassa alimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa, huku akimshukuru mbunge Rdhiwani kwa namna anayoendelea kufanya kazi kubwa za kimaendeleo ndani ya jimbo hilo.

"Nikupongeze mbunge wangu Ridhiwani Kikwete kwa kazi kubwa unayoendelea kuitekeleza ya kiJimbo pia katika nafasi yako ya Unaibu Waziri, hakika rais hajakosea kukuteua katika nafasi uliyonayo, nikuombe tuiangalie shule Mama ina changamoto ya uchakavu ya baadhi ya vyumba vya madarasa," alisema Nassa.

Akijibia hilo Ridhiwani alisema kwamba kwa kuanzia watapeleka kiasi cha shilingi milioni 300, kwa ajili ya kuanza uboreshwaji wa miundombinu hiyo iliyoanza kuchakaa, na kwamba juhudi zaidi zitaendelea ili shule hiyo na nyingine ziwe bora zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji Possi alimhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba kazi itazidi kutekelezwa ndani ya halmashauri ya Chalinze na kwamba fedha zipo za kutosha, pia ina viongozi mahiri na wenye molari wa kuipeleka mbali halmashauri hiyo.

Taarifa ya Afisa elimu shule ya Msingi Miriamu Kihiyo imeelezea mafanikio lukuki katika sekta hiyo, huku akitaja shule ambazo zimefanya vizuri kisha kukabidhiwa fedha ikiwa ni kuunga mkono juhudi za shule husika.

Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri wa Utumishi, Ridhiwani Kikwete (kushoto), akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji Alhaji Ramadhani Possi na Ofisa Habari John Mlyambate

No comments