Header Ads

ad

Breaking News

Wakazi 603 wa Kitunda Relini Gongo la Mboto wafikiwa na huduma ya tiba mkoba

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda akimpima mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya siku tatu iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Jimbo la kati Usharika wa Kitunda Relini na kumalizika mwanzoni mwa wiki hii.


Na Mwandishi Wetu

 WAKAZI 603 wa  Kitunda Relini Gongo la Mboto  jijini Dar es Salaam wamepata huduma za  upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza na homa ya Ini katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanywa na watalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Idara ya magonjwa ya akili na Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Huduma hiyo ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ilifanyika kwa siku tatu na kumalizika hivi karibuni katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani jimbo la Kati usharika wa Kitunda Relini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group na mratibu wa kambi hiyo ya matibabu Samueli Rweyemamu alisema upande wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo watu wazima 216 walifanyiwa vipimo vya moyo.

“Kati ya watu 216 waliofanyiwa vipimo vya moyo watu 110 tumewakuta na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo moyo kutanuka, matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, matatizo ya valvu, shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo hivyo kupewa rufaa ya kufika Hospitali ya JKCI Dar Group kwaajili ya matibabu zaidi,” alisema Dkt. Rweyemamu.

Dkt. Rweyemamu alisema watu 128 walifanyiwa kipimo cha kuchunguza nguvu ya usikivu wa masikio yao watu  26 walikutwa na tatizo la usikivu hafifu ambapo 11 kati yao walipewa rufaa kwaajili ya kuanza matibabu kutokana na hali ya usikivu wa masikio kuwa hafifu sana.

“Tuliangalia ukanda wa Kitunda umepakana na uwanja wa  ndege cha kimataifa wa Julius Nyerere, reli pamoja na maeneo yanayofanya shughuli mbalimbali za jamii ambayo kwa pamoja hutoa sauti kubwa inayoweza kuathiri usikuvu wa wananchi ndio maana tukatoa huduma hii,” alisema Dkt. Rweyemamu.

Upande wa uchunguzi wa magonjwa ya saratani Dkt. Rweyemamu alisema katika kambi hiyo wanawake 227 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti ambapo wanawake wawili waligundulika kuwa na tatizo hilo.

“Uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi ulifanyika kwa wanawake 121 ambapo wanawake 12 wamekutwa na tatizo hilo huku uchunguzi wa tezi dume kwa wanaume umefanyika kwa watu 89 na mmoja kukutwa na tatizo la tezi dume,” alisema Dkt. Rweyemamu.

Dkt. Rweyemamu alisema katika kambi hiyo pia wameweza kufanya uchunguzi na matibabu ya meno na kinywa kwa watu 71, kufanya kipimo cha homa ya ini kwa watu 63 na kutoa chanjo ya homa ya ini kwa watu 50.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema jumla ya watoto 130 walifanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo.

Dkt. Eva alisema watoto 65 walikutwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ikiwemo matundu na mishipa ya damu kutokukaa katika mpangilio wake na  hivyo kupewa rufaa kufika Hospitali ya JKCI Dar Group kwaajili ya matibabu zaidi.

“Kati ya watoto 65 tuliowapa rufaa wapo watoto 20 wenye matundu katika moyo wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo mapema ili kuweza kuziba matundu hayo,” alisema Dkt. Eva.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma ya upimaji katika kambi hiyo waliwashukuru wataalamu wa afya waliotoa huduma hiyo na kusema kuwa imewasaidia kujua afya zao tofauti na ilivyokuwa kabla ya kufanya upimaji.

“Nimepata huduma ya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza  bila gharama zozote zile ninawashukuru wataalamu kwa kutusogezea huduma hii sisi wananchi wenye kipato cha hali ya chini”, alisema Gidion Yona mkazi wa Kitunda.

Gidion alisema kusogeza huduma kwa wananchi kunatoa motisha kwa jamii kuchunguza afya zao kwani ni ngumu mtu kuamua kuifuata huduma ya uchunguzi hospitali  kama hana changamoto zozote za kiafya.

“Nilivyosikia kuhusu huduma hii nilifika hapa kwa haraka kwasababu mimi nina tatizo la shinikizo la juu la damu pamoja na tezi dume hivyo nikaona nishiriki ili niweze kuona maendeleo yangu katika changamoto za kiafya nilizonazo,” alisema Gidion.

“Nimepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo pamoja na dawa bila gharama yoyote ile kwani baada ya kufanyiwa vipimo nilikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, ninawaomba wananchi wanaposikia huduma hizi zinatolewa mahali wasiache kwenda”, alishukuru Hidaya Mohamed mkazi wa Gongo la Mboto.

Afisa Uuguzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Joyce Faustine akimpima wingi wa sukari kwenye damu mkazi wa Kitunda Relini aliyepata huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani jimbo la Kati Usharika wa Kitunda Relini.

Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akitoa elimu ya lishe kwa wakazi wa Kitunda Relini Gongo la Mboto wakati wa kambi maalumu ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani jimbo la Kati Usharika wa Kitunda Relini.

Wakazi wa Kitunda Relini Gongo la Mboto wakisubiri kupata huduma ya matibabu wakati wa kambi maalumu ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani jimbo la Kati Usharika wa Kitunda Relini. Picha na Khamis Mussa.

No comments