Header Ads

ad

Breaking News

Mchujuko Mwenyekiti mpya CHAURU

Mwenyekiti wa Bodi aliyemaliza muda wake, Sadala Chacha akiwa na baadhi ya wajumbe wake


Na Omary Mngindo, Ruvu

WANACHAMA wa Ushirika wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU), mwishoni mwa wiki wamemchagua Mchujuko Tunu kuwa Mwenyekiti mpya wa ushirika huo, atayeuongoza kwa miaka mitatu ijayo.

Kuchaguliwa kwa Mwenyekiti huyo kunamaliza muda wa uongozi uliokuwa chini ya Mwenyekiti Sadala Chacha pamoja na wajumbe wake wa Kamati ya Bodi hiyo.

Kwenye uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Jeshi Kambi ya Ruvu (LoardGuan), ulikuwa chini ya usimamizi wa Ofisa Ushirika, Raphael Kajale aliyepewa jukumu la kuwa msimamizi wa uchaguzi huo.

Kajale alisema kuwa wajumbe wameshiriki kikamilifu uchaguzi huo, huku akimtaja Mchujuko kuwa mshindi kwa kujinyakulia kura 214, makamu wake Otinel Mbura (186), Sade Mwakitalu (173), Renatha Mwaipopo (171) na Shea Bilali kura 154.

"Niwapongeze kwa utulivu tuliouonyesha wakati wa zoezi letu la uchaguzi, tumempata Mwenyekiti wa Bodi, Mchujuko Tunu, Makamu Otiniel Mbura na wajumbe wake, pia tumewapata wajumbe wa kamati nyingine," alisema Kajale.

Akizungumza na waandishi baada ya uchaguzi huo, Mchujuko aliwashukuru wajumbe kwa kuonesha imani kwake na wenzake huku akiahidi kuwatumikia kwa moyo wao wote.

Naye, Mwenyekiti mstaafu Chacha aliwaambia waandishi kwamba, katika kipindi cha uongozi, wameongoza kwa mafanikio makubwa, huku akiwaomba viongozi wapya washirikiane na wanachama kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana.

 Ofisa Ushirika Raphael Kajale, ambaye katika zoezi hilo alikuwa msimamizi wa uchaguzi, akitangaza matokeo.
Baadhi ya wanachama wa CHAURU wakifuatilia uchaguzi huo. Picha zote na Omary Mngindo

No comments