Header Ads

ad

Breaking News

FCC, CTI WASAINI USHIRIKIANO WA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA KWA MLAJI NCHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) Leodegar Tenga (kulia), akisaini mkataba kati ya CTI na Tume ya Ushindani nchini (FCC). Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa (FCC) William Erio mapema leo Juni 5,2025, Jijini Dar es Salaam.


NA ANDREW CHALE, DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Ushindani (FCC), imeendelea kuhakikisha inamlinda mlaji nchini hususani bidhaa zinazotoka katika viwanda vya ndani na vile vya nje katika kudhibiti bidhaa bandia.

Hayo yamebainishwa Juni 5,2024 katika tukio maalum la utiliaji wa saini mashirikiano na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), katika utendaji wa kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda na kudhibiti uzalishaji wa bidhaa bandia.

Tukio hilo la kusaini makubaliano hayo, limefanyika mapema Juni 5, 2024 baina ya Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio na Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Mhandisi Leodegar Tenga jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la kusaini makubaliano hayo ni kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi kukuza viwanda na kudhibiti bidhaa bandia.

“Kusainiwa wa makubaliano haya kutawezesha kufikia malengo ya serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.Mahusiano haya yatahusu namna bora ya kubadilishana taarifa hususan utekelezaji wa sheria mbili ambazo FCC tunazisimamia ikiwemo ya Ushindani na ya alama au nembo ya bidhaa zinazowahusu wenye viwanda,” amesema.

Amesema katika majukumu ya CTI kupitia sera na dira zao zinaonyesha ambavyo wanalenga kulinda mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini kwa wenye viwanda kufikia matarajio yao na kukuza uchumi wa viwanda.

Aidha, Erio, amesema wanaendelea kulinda na kushabihisha ushindani, hivyo wanahakikisha wanadhibiti vitu ambavyo vinaweza kuathiri wawekezaji hao ikiwemo ukiukaji wa sheria na makubaliano kuhakikisha havifanyiki.

Akielezea kuhusu sheria ya bidhaa bandia amesema, inazuia kupitia mipaka ya nchi na kutozalishwa nchini, ndiyo maana wamesaini makubaliano hayo kuhakikisha wanalinda uzalishaji huo wenye tija katika kukuza ajira, fursa ya uchaguzi wa bidhaa na kukuza uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Mhandisi  Tenga, ameipongeza FCC kwa kufanikisha kusainiwa kwa makubaliano hayo yanayotokana na ushirikiano mzuri wa Taasisi hizo mbili.

Amesema kufanikiwa kwa makubaliano hayo ni fursa kubwa ya kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji wa viwanda yanalindwa na kufikia azma ya serikali ya sekta hiyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mkurugenzi Erio amesema kupitia CTI, watakubaliana kuwa na umoja wao uliosajiliwa wa kulinda nembo za bidhaa zao zisiibiwe na kutumia na wengine bila kibali, akitolea mafanikio kwa mataifa yaliyoendelea ikiwemo Marekani walivyofanikiwa katika hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) Leodegar Tenga (kulia), wakibadilishana nyaraka za mkataba kati ya CTI na Tume ya Ushindani nchini (FCC). Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa (FCC), William Erio wakati wa utiliaji saini mapema leo Juni 5,2025, Jijini Dar es Salaam.

No comments