Header Ads

ad

Breaking News

ALICHOKISEMA MSAJILI WA HAZINA KATIKA HOTUBA YAKE WAKATI WA HALFA YA SIKU YA GAWIO 2024

 

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

MSAJILI WA HAZINA, Nehemiah Kyando Mchechu, amesema ofisi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kushawishi kufanyika kwa reforms katika sheria yake ili kuanzishwa kwa mamlaka ya uwekezaji wa umma. 

Mchechu aliyasema hayo wakati wa halfa ya Siku ya Gawio 2024 wa lengo la kupokea gawio kutoka katika mashirika na asisi za umma na kampuni ambazo serikali na hisa zake, Juni 11,2024.

Alisema kuwa, kwa hatua waliyofikia, alimshukuru Waziri Profesa Kitila  Mkumbo kwa kujitoa kwake na ari aliyoionesha kwenye kuandaa na kuhakikisha muswada huo unapita

Msajili wa Hazina alisema kuwa, ni imani yake, baada ya muswada kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 2023 utaendelea na hatua zinazofuata,huku wakiamini wapo kwenye njia sahihi ya kuhakikisha mabadiliko yanafanikiwa kupitia sheria mpya ya mamlaka ya uwekezaji wa umma. 

"Ni wazi kuwa, tunahitaji sheria inayojitosheleza itakayoweza kusaidia kuleta tija katika uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi trilioni 76  uliofanywa na Serikali kwa niaba ya umma wa Watanzania," alisema Msajili wa Hazina.

Alisema kuwa, Msajili wa Hazina amefanya mkutano na mafunzo kwa wakurugenzi wanaowakilisha kwenye kampuni ambazo wana umiliki wa hisa chache.

Mchechu alisema kuwa, mafunzo hayo yalikuwa na umuhimu mkubwa chini ya kaulimbiu ya “Uzalendo wa Kiuchumi katika uwekezaji wa Umma”, ambapo sehemu ya matokeo ya walichokiona wakati wa hafla ya gawio ni matokeo ya mafunzo hayo.

Aliongeza kuwa, wameendelea na mafunzo ya wakurugenzi wa Bodi kwenye Mashirika ya Umma kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi, ambapo kuanzia mwaka ujao wa fedha wataanza na mafunzo maalum (Induction Course) kwa kundi la watendaji wakuu wapya walioteuliwa ndani ya kipindi cha miaka miwili kama sehemu ya kuimarisha utendaji kazi wa mashirika haya.

Mchechu alisema katika kuimarisha utawala bora na tija ya mashirika ya umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina imezindua na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kufanya tathmini ya bodi, hali ambayo imewezesha kukamlisha tathmini kwa wakati na kwa mawanda tarajiwa.

 Aidha, Ofisi hiyo imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika (Key Performance Indicators) vilivyoingiwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina. 

Msajili wa Hazina alisema kuwa, vgezo hivyo vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi na wataendelea kuboresha vigezo hivyo mara kwa mara, kwa kutegemea mrejesho kutoka taasisi zao hizo ambao ndiyo wadau wetu.

Aliongeza kusema kuwa, wapo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti (dashboard) taarifa za kiutendaji za wakuu wa taasisi kwa wakati na za kuaminika ili kuwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati (informed decision making) kwa mamlaka za uteuzi.

"Ofisi imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia wetu kwenye sekta nyeti za Uchumi,  kwenye sekta ya madini kumekuwa na mzungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini na tumeweza kuongeza hisa za serikali katika baadhi ya kampuni, mathalani tumeongeza hisa za serikali katika Kampuni ya Madini ya Sotta kutoka asilimia 16 hadi asilimia 20, jambo hili litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo."

"Pia, tumekamilisha majadiliano na kuingia mipya ya wanahisa na makampuni kama NMB, NBC na MCCL kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza hatimaye kupata faida mwaka huu na kutoa Gawio kwa wanahisa Mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10," amesema Msajili wa Hazina.

Mchechu aliyataja mambo mengi ambayo yamefanyika katika kuitikia wito wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kutekeleza maono yake ya kuleta mageuzi katika utendaji kazi mahali popote penye uwekezaji wa umma.

Alimweleza Rais Dkt. Samia kuwa, siku ya gawio kulikuwa na wawakilishi wa mashirika yasiyopungua 300, yakiwakilishwa na wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu. 

Aliongeza kuwa, jumla ya mashirika yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina mpaka sasa ni 304, katika mgawanyiko wa yale ambayo wana asilimia nyingi za umiliki. 

Mchechu alisema  kuwa,kama, Serikali (majority shareholding) ambayo ni 248 na yale ambayo wana hisa chache “minority interest” ambayo ni 56, amemweleza Rais kuwa, siku ya gawio  atapokea jumla ya shilingi 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio shilingi 278,868,961,122.85 kutoka katika mashirika ya biashara na michango shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine. 

"Makusanyo haya ni kwa kipindi kinachoanzia Julai 2023 hadi Mei 2024. Hata hivyo, kwa kuwa mwaka wa fedha wa 2023/24 bado haujakamilika, makusanyo bado yanaendelea, na tunatarajia kufikisha kiasi cha shilingi bilioni 850. Hivyo, alitoa rai kwa wale ambao wanadaiwa au hawajatoa kuhakikisha kuwa wanakamilisha malipo yao kabla ya mwisho wa Mwaka huu wa fedha.

Alisema jumla ya mashirika yaliyochangia katika kipindi hiki ni 145 ambalo ni ongezeko la mashirika 36 kutoka 109 ya mwaka jana, aidha mashirika 159 hayajachangia kabisa katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka huu.

Mchechu aliongeza kuwa, idadi hiyo sio ndogo, hivyo wanatoa wito kuwa taasisi zote zibadilike na kuboresha utendaji wao wa kazi utakaowawezesha kuanza kuchangia ama kuongeza uchangiaji katika mfuko mkuu wa serikali. 

"Kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali sio suala la kujitolea au fadhila kwa Serikali, bali ni wajibu wa lazima. Kwa kuzingatia uwekezaji wa Serikali katika mashirika ambao unafikia shilingi trilioni 76 hadi sasa, kiasi cha gawio na michango kinachokusanywa hadi sasa sio cha kuridhisha na tunaamini kuwa, waliokabidhiwa kuongoza mashirika haya, wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa faida ya taifa na wananchi wote kwa ujumla. 

"Mwenendo wetu sio mzuri sana kama tunataka kuyafikia malengo uliyotupatia mwaka jana ya kuhakikisha kuwa tunafikia asilimia 10 ya mapato ya kikodi, na nayasema haya hapa mbele yako Mheshimiwa Rais nikiamini kuwa wahusika wote hapa tulikuelewa vizuri mwaka jana na kuwa tutachukua hatua za dhati kabisa ili kuleta mabadiliko chanya na ya haraka katika mashirika haya na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa nchi yetu."

Alisema kuwa, ili kufikia lengo tarajiwa la kuona kuimarika kwa mchango wa mashirika ya umma na taasisi ambazo kuna uwekezaji wa Serikali katika kujenga uchumi na maendeleo endelevu ya nchi, hivyo mabadiliko ya kiusimamizi, kiutendaji na kiuendeshaji hayaepukiki.


Hotuba kamili hapo chini;


HOTUBA YA NDUGU NEHEMIAH KYANDO MCHECHU, MSAJILI WA HAZINA WAKATI WA HALFA YA SIKU YA GAWIO 2024 KWA LENGO LA KUPOKEA GAWIO KUTOKA MASHIRIKA NA TAASISI ZA UMMA NA KAMPUNI AMBAZO SERIKALI INA HISA CHACHE.

TAREHE 11 JUNI, 2024, IKULU DAR ES SALAAM


Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Dotto Biteko (Mb.), Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati;

Mheshimiwa DKt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,

Mheshimwa Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wengine mliohudhuria hapa,

Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge,

 

Balozi Moses Mpogole Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu,

Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama,


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,

 

Viongozi Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi. Waheed Muhammad Sanya, Msajili wa Hazina Zanzibar, Wageni waalikwa,

Mabibi na mabwana,

 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

 

 Mheshimiwa Rais na Mgeni Rasmi,

 Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima kuwa hapa siku hii ya leo ikiwa ni siku ya kipekee kabisa ya kukabidhi gawio kutoka mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina hisa chache. Aidha nikushukuru wewe Mheshimiwa Rais kwa njia ya kipekee kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika shughuli hii muhimu ya kupokea gawio, fedha ambazo ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Lakini nakushukuru zaidi kwa kukubali shughuli hii kufanyika hapa Ikulu hapa Dar es Salaam. Kujitoa muda wako na kuruhusu kufanyika hafla hii hapa Ikulu ni kielelezo tosha cha wewe kujitoa kwako katika mageuzi ya kiutendaji uliyoyaanzisha na Imani yako uliyonayo kwenye mashirika yetu ya umma kwa maslahi ya nchi yetu.

 Mheshimiwa Rais,

 Kauli mbiu ya zoezi hili la gawio kwa mwaka huu ni “mageuzi ya mashirika ya umma na wajibu wa kuchangia maendeleo ya Tanzania”. Kauli mbiu hii tumeiweka kuakisi umuhimu wa kuimarisha utendaji kazi katika mashirika na sehemu zote zenye uwekezaji wa Serikali na


pia kutimiza wajibu wao wa kuchangia maendeleo ya nchi yetu kupitia gawio na michango ambao ni zao la uwekezaji uliofanywa na Serikali.

 Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

 Nasimama hapa ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuambatana na viongozi wa taasisi zote hizi kuja kuwasilisha gawio la ujumla kwako kutoka katika mashirika na taasisi zote ambazo Serikali ina uwekezaji tangu uniteue kuwa Msajili wa Hazina. Ninaelewa kuwa mwaka 2023 niliwasilisha gawio kutoka kwa taasisi moja. Hata hivyo, tofauti na mwaka jana, mwaka huu tumeona tuanze utamaduni wa kuyaleta mashirika pamoja na kufanya matukio ya msingi kwa pamoja. Utamaduni wa kwenda pamoja tunautimiza kama ulivyoagiza tarehe 11 Disemba 2023 wakati tulipowasilisha michango ya mashirika ya umma kwenye kusaidia janga la maporomoko ya Hanang. Ni ahadi yetu kuwa tutaendeleza umoja huu kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

 Mheshimiwa Rais,

 Leo ni siku maalum kwa ajili ya Serikali kupokea gawio kama faida ya uwekezaji wa Serikali kwenye mashirika ya umma na binafsi. Kwa kuwa ni siku mahsusi ya gawio, na kwa faida ya wote ninaomba nitaje kwa ufupi baadhi ya vifungu vya sheria vinavyotoa wajibu wa mashirika na taasisi za umma kutoa gawio na michango;

1.     Kifungu cha 8(f) cha Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina SURA 370, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 11(3) cha Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 vimeweka wajibu kwa Wakala


wa Serikali, Mashirika na Taasisi za umma kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi katika mfuko mkuu wa Serikali;

2.     Kifungu cha 7 cha Sheria ya Mashirika ya Umma SURA 257, pamoja na mambo mengine, kimeelekeza Mashirika ya Umma kujiendesha kwa misingi thabiti ya kibiashara na kupata rejesho la mtaji lisilopungua asilimia 5, na kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali;

3.     Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, kifungu cha 10(2)(i) kinatoa wajibu kwa Msajili wa Hazina Kufuatilia na kuhakikisha michango na gawio kutoka katika Mashirika ya umma inalipwa kwa wakati;

4.     Kifungu cha 10A(1) cha sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina kimeweka masharti ya mashirika ya umma kupuguza matumizi ambapo mashirika hayo yanatakiwa kutumia sio zaidi ya asilimia 60 ya mapato baada ya kutoa gharama ya mishahara na bakaa inayopatikana baada ya matumizi hayo kuwekwa katika mfuko mkuu wa Serikali;

 Mheshimiwa Rais,

 Kwa kuwa hii ni hafla ya kipekee kuhusu mashirika ya umma naomba uniruhusu pia kupitia umma huu niseme machache ya baadhi ya majukumu tuliyoyafanya ambayo ni sehemu ya kufika siku hii ya leo;

Kwanza, ofisi ya msajili wa hazina imeendelea kushawishi kufanyika kwa reforms katika sheria yake ili kuanzishwa kwa mamlaka ya uwekezaji wa umma. Kwa hatua tuliyofikia, naomba nimshukuru Waziri wetu Profesa Kitila Alexander Mkumbo kwa kujitoa kwake na ari aliyoionesha kwenye kuandaa na kuhakikisha muswada huu unapita


kama ulivyoelekeza. Ni imani yetu, baada ya muswada kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 2023 utaendelea na hatua zinazofuata. Aidha tunaamini tupo kwenye njia sahihi ya kuhakikisha mabadiliko yanafanikiwa kupitia sheria mpya ya mamlaka ya uwekezaji wa umma. Ni wazi kuwa tunahitaji sheria inayojitosheleza itakayoweza kusaidia kuleta tija katika uwekezaji mkubwa wa zaidi ya TZS 76 Trilioni uliofanywa na Serikali kwa niaba ya Umma wa Watanzania.

La pili, Msajili wa wa hazina imefanya mkutano na mafunzo kwa wakurugenzi wanaotuwakilisha kwenye kampuni ambazo tuna umiliki wa hisa chache. Mafunzo haya yalikuwa na umuhimu mkubwa chini ya kaulimbiu ya “Uzalendo wa Kiuchumi katika uwekezaji wa Umma”. Sehemu ya matokeo ya tutakachokiona leo ni matokeo ya mafunzo haya. Pia tumeendelea na mafunzo ya Wakurugenzi wa Bodi kwenye Mashirika ya Umma kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi. Na kuanzia mwaka ujao wa fedha tutaanza na mafunzo maalum (Induction Course) kwa kundi la Watendaji Wakuu wapya walioteuliwa ndani ya kipindi cha miaka miwili kama sehemu ya kuimarisha utendaji kazi wa mashirika haya.

La tatu, katika kuimarisha utawala bora na tija ya mashirika ya umma, Ofisi imezindua na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kufanya tathmini ya bodi hali ambayo imewezesha kukamlisha tathmini kwa wakati na kwa mawanda tarajiwa. Aidha Ofisi imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika (Key Performance Indicators) vilivyoingiwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina. Vigezo hivi vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi, na tutaendelea kuboresha vigezo hivi mara kwa marana pia kwa kutegemea mrejesho kutoka taasisi zetu hizi ambao ndio wadau wetu.


La nne, tupo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti (dashboard) taarifa za kiutendaji za wakuu wa taasisi kwa wakati na za kuaminika ili kuwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati (informed decision making) kwa mamlaka za uteuzi.

Ofisi pia imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia wetu kwenye sekta nyeti za Uchumi; kwenye sekta ya madini kumekuwa na mzungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini na tumeweza kuongeza hisa za serikali katika baadhi ya Kampuni, Mathalani tumeongeza hisa za serikali katika Kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo. Pia tumekamilisha majadiliano na kuingia mipya ya wanahisa na makampuni kama NMB, NBC na MCCL kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza hatimaye kupata faida mwaka huu na kutoa Gawio kwa wanahisa Mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10.

Mheshimiwa Rais kuna mambo mengi ambayo yamefanyika katika kuitikia wito wako na kutekeleza maono yako ya kuleta mageuzi katika utendaji kazi mahali popote penye uwekezaji wa Umma, lakini itoshe kusema kuwa leo sio siku yetu ya kuzungumzia tuliyoyafanya kwakuwa leo ni siku maalam ya kupokea gawio (Tanzania Dividend Day)

 Mheshimiwa Rais,

Mbele yako tuna wawakilishi wa mashirika yasiyopungua 300, yakiwakilishwa na wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu. Jumla ya mashirika yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina mpaka sasa ni 304, katika mgawanyiko wa yale ambayo tuna asilimia nyingi za umiliki


kama Serikali (majority shareholding) ambayo ni 248 na yale ambayo tuna hisa chache “minority interest” ambayo ni 56. Siku ya leo unapokea jumla ya shilingi 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio shilingi 278,868,961,122.85 kutoka katika mashirika ya biashara na michango shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine. Makusanyo haya ni kwa kipindi kinachoanzia Julai 2023 hadi mwezi Mei 2024. Hata hivyo kwa kuwa mwaka wa fedha wa 2023/24 bado haujakamilika, makusanyo bado yanaendelea, na tunatarajia kufikisha kiasi cha shilingi bilioni 850. Hivyo, naomba kupitia hadhara hii na mbele yako Mheshimiwa Rais, nitoe rai kwa wale ambao wanadaiwa au hawajatoa kuhakikisha kuwa wanakamilisha malipo yao kabla ya mwisho wa Mwaka huu wa fedha.

 Mheshimiwa Rais,

 Jumla ya mashirika yaliyochangia katika kipindi hiki ni 145 ambalo ni ongezeko la mashirika 36 kutoka 109 ya mwaka jana. Aidha mashirika 159 hayajachangia kabisa katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka huu. Idadi hii sio ndogo, hivyo tunatoa wito kuwa taasisi zote zibadilike na kuboresha utendaji wao wa kazi utakaowawezesha kuanza kuchangia ama kuongeza uchangiaji katika mfuko mkuu wa serikali. Kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali sio suala la kujitolea au fadhila kwa Serikali, bali ni wajibu wa lazima. Kwa kuzingatia uwekezaji wa Serikali katika mashirika ambao unafikia shilingi trilioni 76 hadi sasa, kiasi cha gawio na michango kinachokusanywa hadi sasa sio cha kuridhisha na tunaamini kuwa waliokabidhiwa kuongoza mashirika haya, wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa faida ya taifa na wananchi wote kwa ujumla. Mwenendo wetu sio mzuri sana kama


tunataka kuyafikia malengo uliyotupatia mwaka jana ya kuhakikisha kuwa tunafikia 10% ya mapato ya kikodi, na nayasema haya hapa mbele yako Mheshimiwa Rais nikiamini kuwa wahusika wote hapa tulikuelewa vizuri Mwaka jana na kuwa tutachukua hatua za dhati kabisa ili kuleta mabadiliko Chanya na ya haraka katika mashirika haya na hivyo kusaidia kukuza Uchumi wa nchi yetu. Ieleweke kuwa, ili kufikia lengo tarajiwa la kuona kuimarika kwa mchango wa mashirika ya umma na taasisi ambazo kuna uwekezaji wa Serikali katika kujenga uchumi na maendeleo endelevu ya nchi, basi mabadiliko ya kiusimamizi, kiutendaji na kiuendeshaji hayaepukiki.

 Mheshimiwa Rais,

 Ilituchukua takribani miaka thelathini kwa nchi yetu kufanya mageuzi ya uendeshaji wa Mashirika yetu chini ya usimamizi wa IMF na WB kutokea baada ya Uhuru na Muungano wa nchi zetu, na sasa tunashukuru kuwa miaka thelathini baadaye Mheshimiwa Rais, umeanzisha mageuzi kwa awamu ya pili, bila kusubiri kuambiwa ama kusurutishwa na mabwana wakubwa hawa. Mheshimiwa Rais, niseme ya kuwa mimi na viongozi wenzangu tuliohudhuria hafla hii na kwaniaba ya wengine ambao hawapo katika hadhara hii, ya kuwa hatutakuangusha katika dhamira na maono yako haya. Na matokeo ya mageuzi yatakuwa ni kuimarika kwa ubora wa huduma zetu kwa wananchi, wadau na wateja wetu, kuongezeka kwa faida na hivyo mchango wetu katika mfuko mkuu wa Taifa, na mwisho kupunguza mzigo wa utegemezi kutoka mfuko mkuu kwa taasisi ambazo sio za kutengeneza faida au ziada kubwa katika shughuli zao. Tunatambua mchango wa taasisi zisizo za kibiashara, lakini wao tutawazungumzia tukiwa kwenye kikao chetu cha Arusha, kwakuwa leo ni siku ya kitaifa ya Gawio la Serikali.

 Mheshimiwa Rais,

 Miaka ya nyuma, kiasi kikubwa cha gawio kutoka katika mashirika ya biashara (Dividend) kilikuwa kinatoka katika mashirika ya umma. Mfano kati ya mwaka 2019/20 hadi 2021/22 mashirika ya umma yalichangia kiasi cha shilingi bilioni 255.8, 161.6, na 207.2 mtawalia, ambapo kampuni ambazo serikali ina hisa chache zilichangia kiasi cha shilingi bilioni 44.3, 147.2 na 150.3 mtawalia. Hata hivyo, mizania ya uchangiaji kwa sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa ambapo asilimia kubwa ya gawio linatoka kwenye kampuni ambazo Serikali ina hisa chache. Mathalani katika kipindi cha miaka miwili 2022/23 na 2023/24 gawio la mashirika ya umma yanayofanya biashara, ilikuwa shilingi bilioni 109.7 na 110.3 mtawalia, ambapo kampuni ambazo serikali ina hisa chache zilichangia kiasi cha shilingi bilioni 219 na bilioni 168 mtawalia katika kipindi hicho. Na kwa Mwaka huu, katika msimamo wa makampuni ya kibiashara yaliyofanya vizuri na kurejesha faida nzuri serikalini, nafasi kumi bora za juu zimeshikiliwa na makampuni ambayo tuna hisa chache (Minority Shareholding).

 Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Matokea haya kwetu yanaleta fikra mchanganyiko (mixed feelings) na ni wake up call kwetu kwa taasisi zetu za umma. Ni habari njema kwa kuwa inaonesha wazi uwezeshaji unaofanywa na serikali yako ya awamu ya sita katika kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara yanafanikiwa kwa kampuni binafsi kufanya kazi nchini Tanzania na kupata faida. Mheshimiwa Rais, Faida katika biashara za sekta binafsi ni kipima joto cha uhakika cha mafanikio ya serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na sera nzuri za kiuchumi katika nchi husika, Faida ni tunda la Biashara na leo hesabu zinaongea kwa urahisi juu ya kuimarika na kuboreka kwa mazingira ya biashara nchini, ambayo kimsingi ni safari na sio kituo kwamba ukifika unatulia.

Lakini pia hali hii inaonesha kuwa kuna somo ambalo sisi kama Serikali tuna kila sababu ya kujifunza kwa namna taasisi zetu za umma zinavyoendeshwa, na kujiuliza kulikoni Taasisi za biashara ambazo umiliki mkubwa ni serikali hatupo kwenye kumi bora (top ten) katika faida na uchangiaji wa gawio serikalini? Kwahiyo, kuna somo ambalo tunapaswa kujifunza na hivyo kulihuisha kwenye mashirika yetu ya umma ambapo Serikali ina umiliki wa hisa nyingi, na wenzetu huko tuliko na hisa chache wanatembea katika safari ya mabadiliko na maboresho kila mwaka sambamba na maagizo yako kwetu kwenye 4R na hususani Reforms & Rebuilding.

Katika kuhakikisha tunatumia uzoefu wa taasisi hizi ambazo uchangiaji wake unakua kwa kasi, na kwa kuhakikisha maslahi ya Serikali yanalindwa, tumeanza utaratibu wa kufanya vikao kazi vya pamoja ambavyo ni ziada ya vikao vya kawaida vya kiuendeshaji. Mwezi Machi 2024 katika shule ya ualimu Mwalimu Nyerere Kibaha, tuliandaa kikao kazi mahsusi kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na wakurugenzi wanaoiwakilisha Serikali katika Bodi za MIs. Kikao kazi hiki pia kilihusisha wakurugenzi wakuu wa taasisi hizo ili kuendelea kubadilisha uzoefu na kuongeza tija, na tayari tumeanza kuona matokeo ya intiatives hizi. Utaratibu huu ni endelevu na utakuwa ukifanyika kila mwaka kama ambavyo tutakavyokuwa tunaendelea na kikao kikuu kazi kwa Taasisi za Umma kinachofanyika mwezi August kila mwaka na kwa Mwaka huu tutakuwa Arusha tena.

 Mheshimiwa Rais,

 Pamoja na kutoa gawio katika mfuko mkuu wa Serikali, mashirika yana faida pia katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa ajira, kutoa huduma za msingi na wezeshi hata maeneo ambayo yasipata huduma kama kusingalikuwa na mashirika ya Umma, kubeba miradi ya maendeleo katika sekta zote za uchumi, kuchangia katika pato la taifa nk. Ni nia thabiti ya Ofisi hii kuhakikisha kuwa faida hizi zinakuwa imara, endelevu na zinaendelea kuongezeka kila mara.

 Mheshimiwa Rais,

 Sisi tunaamini kuwa kupitia falsafa yako ya 4Rs ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina na mashirika imejikita katika R2 za reforms na rebuilding, historia itakukumbuka wewe kuwa “Mama wa Taifa letu msimamizi wa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo nchini Tanzania”. Na ni kwa sababu hiyo nasi tumejipanga kuhakikisha ufanisi wa mashirika na taasisi zote za umma unaendana na maono yako ya kuitengeneza sekta ya umma ambayo inachochea na kushikamana kikamilifu na taasisi binafsi nje na ndani ya nchi kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi duniani.

Kwasasa kama ofisi ya Msajili wa Hazina, tumejikita kufanya tathmini ya kina ya mipango mkakati, mpango wa mwaka, na bajeti ya mwaka kwa taasisi zetu hizi na lengo likiwa ni kutoa ushauri wa kimkakati kwa taasisi zetu pamoja na kupitia upya malengo, vigezo vya upimaji kazi na kiwango watakachotakiwa kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali. Pamoja na hilo, pia tumedhamiria kufanya makubaliano ya muda wa mwisho wa kuendelea kuitegemea serikali kwa baadhi ya Taasisi ambazo kwa namna moja ama nyingine bado zinautegemezi wa bajeti ya Serikali kwakuwa nao ni sehemu ya mchango serikalini, na katika hili naomba niwapongeze TPDC na STAMICO ambao mwaka jana tuliingia makubaliano ya kuwa watapewa mwaka mmoja tu wa kuendelea kuitegemea serikali katika baadhi ya gharama za uendeshaji na ambao kwa Mwaka huu wamejitoa na sasa watajitegemea kwa 100% ya gharama za uendeshaji. Kwahiyo, nawaomba Wenyeviti na Watendaji wakuu wa Taasisi za Umma, tuanze kuzoea mahitaji ya mabadiliko (push back) ya bajeti zenu kutoka OMH na ambayo mtaletewa yakiwa na uchambuzi wa kina.

 Mheshimiwa Rais,

 Kabla ya kumaliza, naomba nikushukuru kwa mara nyingine kwa siku hii lakini kwa ridhaa yako naomba kuwasilisha maombi mawili mbele ya hadhara hii. Ombi la kwanza ni kuhusu hii siku ya leo, ikikupendeza tunaomba siku hii ijulikane kama “Siku ya Gawio Tanzania” au “Tanzania Dividend Day” itakayofanyika kila mwaka na pendekezo letu ukiona inafaa iingie kwenye ratiba ya ofisi yako kufanyika kila wiki ya mwisho ya mwezi Mei au wiki ya kwanza ya mwezi Juni; Huko makanisa siku kama hii huitwa ni SikuKuu ya mavuno.

Ombi la pili Mheshimiwa Rais, ni kuhusu kikao kikuu cha kila mwaka cha wakuu wa Taasisi zilizopo mbele yako pamoja na wenyeviti wao wa bodi. Utakumbuka kuwa mwaka jana tulifanya kikao Maalum cha Mwaka mwezi Agosti na tunashukuru uliridhia kuwa mgeni rasmi na kikawa na manufaa makubwa. Ombi letu kwa mwaka huu pia tunaomba kwa heshima na taadhima uridhie kuwa mgeni rasmi katika mkutano na wakuu hawa wa Taasisi za Umma na Wenyeviti wao. Tayari maandalizi yameshaanza na tumelenga wiki ya pili ya mwezi Agosti kama ratiba yako ikiruhusu. Huko tutakuwa na majadiliano ya kina ya namna ya kufanya mageuzi na mabadiliko makubwa ya kiutendaji ili kufikia maono yako. Mwaka jana ulituachia pia changamoto ya kuangalia ni namna gani mashirika ya umma ya Tanzania yanaweza kutoka nje ya mipaka na kufanya biashara na kurejesha faida nyumbani. Tunaona mashirika ya Umma kutoka baadhi ya nchi yanavyofanya biashara kubwa nje ya nchi zao ikiwamo ndani ya mipaka ya Tanzania na tunatamani katika kipindi chako cha Uongozi walao tuweze kuwa na Mashirika kadhaa yanayoendesha shughuli zake nje ya mipaka ya nchi yetu, kwahiyo, hilo ni jambo ambalo pia tuanedelea kulizingatia.

 Mheshimiwa Rais,

 Na mwisho naomba nitoe ufafanuzi juu ya zoezi utakalolifanya baadaye la kupokea hundi za mfano kwaajili ya michango na gawio la faida. Uchangia upo katika namna mbili, ya kwanza ni kwa taasisi za biashara ambazo zinatakiwa kutoa sehemua ya gawio la faida kwa wanahisa wake, na katika kundi hili tumechanganya wachangiaji wote bila kujali kama umiliki mkubwa ni wa serikali au ni kule kwenye hisa ndogo. Na pili kuna taasisi zetu ambazo sio za biashara kwa kazi zao, lakini zina makusanyo au vyanzo vya mapato katika shughuli zao, na taasisi hizi hutakiwa kuchangia 15% ya mapato yao ghafi. Kwa makundi yote mawili watakaopata nafasi ya kutoa hundi ya mfano kwako Mheshimiwa Rais, ni wale tu waliotoa zaidi ya TZS 10b. Na hiki ndio kiwango ambacho kitakuwa ndio kiwango cha chini hata kwa mwakani na natumaini mwaka ujao tutakuwa na watu wengi watakaokuwa wamechangia zaidi ya TZS 10b na kwamba wote watapata nafasi ya kutambuliwa nawe Mheshimiwa rais na pia kuonekana kwa Watanzania wengi. Na kwa Mwaka huu imetokea kuwa na Taasisi tano kwa kila upande kama ambavyo wataitwa hapo baadaye.

Kwa taasisi za kibiashara, Kundi hili linajumuisha Mashirika na Kampuni ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya umma na Sheria ya Makampuni, zinawajibika kutoa gawio kwa wanahisa, na zilitoa gawio zaidi ya bilioni kumi ni; 1)NMB; (Tzs 54.5bn); 2)Twiga Minerals (Tzs 53.4bn); 3)Airtel Tanzania (Tzs 40.8bn); 4)Puma Energy (Tzs 12.2bn); 5)TPC Moshi (Tzs 10.2bn)

Kwa taasisi zisizo za biashara, Kundi hili linajumuisha Mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina na sheria ya Mashirika ya umma zinawajibika kutoa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, na taasisi zilizotoa zaidi ya bilioni kumi ni; 1)TPA; (Tzs 153.9bn);  2)TCRA (Tzs 34.7bn);  3)TFS (Tzs 21.3bn);  4)TASAC (Tzs 19.1     bn); 5)BRELA (Tzs 18.9bn)

 

Pia kutakuwa na Tuzo tano kama ambavyo tutaletewa maelezo yake hapo baadaye, na tuzo hizo zitawahusisha

1.     Wachangiaji wakubwa watatu wa gawio

2.     Wachangiaji wakubwa watatu wa michango ya 15%

3.     Taasisi zilizofanya mabadiliko makubwa katika utendaji na kuwezesha kutoa gawio na michango kwa uwiano mkubwa ukilinganisha na kipindi kilichopita

        4.     Taasisi ambazo kwa kipindi chote zimekuwa zikichangia consistently, kwa wakati na               kwa kiasi stahiki.

         5.     Taasisi ambazo zimefanya mageuzi makubwa ya kiutendaji na kiundeshaji na hivyo                  kuziwezesha kuchangia kwa mara ya kwanza na kwa kiasi ambacho ni stahiki baada                ya miaka mingi.

 Mheshimiwa Rais, kwa heshima na taadhima nakushukuru sana na asanteni kwa kunisikiliza.

No comments