Header Ads

ad

Breaking News

Wakazi Vikuruti wafurahia kuzinduliwa zahanati

Mganga Mkuu wa Halmashauri Kibaha, Wilford Kondo 


Na Omary Mngindo, Mlandizi

WAKAZI wa Kitongoji cha Vikuruti Kata ya Mlandizi Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wamefurahia kuzinduliwa kwa zahanati iliyopo katika kitongoji chao.

Salehe Kawambwa na Aisha Hassan ambao ni wakazi wa kitongoji hicho kwa niaba ya wenzao walisema kuwa,  kuzinduliwa kwa zahanati hiyo na Mbio za Mwenge Mei Mosi ni mkombozi, kwani awali walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma.

"Tunaishukuru Serikali kwa kazi kubwa ya kutujengea zahanati hapa Vikuruti, itakuwa mkombozi kwani kwa miaka mingi tulikuwa tunakwenda Mbwawa, Kambi ya Ruvu JKT au Mlandizi lakini kwa sasa tutapata huduma hapahapa," alisema Kawambwa za matibabu.

Kwa upande wake Aisha alisema kuwa, amefika katika zahanati hiyo kumpima mtoto wake, huduma ambayo kabla ya ujenzi huo alikuwa akiipata katika Kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi au Mbwawa kwa gharama ya zaidi ya shilingi elfu tano 5,000, kwani walikuwa wakitumia usafiri wa pikipiki.

"Kabla ya zahanati hii, nikiwa nataka kumpima mtoto nilikuwa nalazimika kukodi pikipiki kwa gharama ya shilingi 5,000 kwenda Mbwawa, Mlandizi au Zahanati ya jeshi JKT Ruvu," alisema Aisha.

Mganga Mkuu wa Halmashauri Kibaha, Wilford Kondo alimwelezea kiongozi wa mbio za mwenge kwamba, ujenzi wa zahanati hiyo ulianza Aprili Mosi mwaka 2022 kwa ujenzi wa jengo la nje OPD.

"Ujenzi ulitekelezwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri, ulianza Aprili Mosi,2022 kwa kujenga jengo la nje yaani OPD, mwaka wa fedha 2022 tulipokea shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi  na mwaka 2023 tulipokea tena shilingi milioni 100."

Dkt. Kondo aliongeza kuwa, kuna nguvu za wananchi za shilingi milioni 2.5, ambapo Juni 15,2023 kituo kilitembelewa na mbio za mwenge wa Uhuru, chini ya kiongozi wake Abdallah Shaibu na kuwekewa jiwe la msingi.

"Ujenzi wa huduma za nje ulikamilika Septemba 2023, zahanati ilipokea vifaa kutoka Bohari ya Dawa ikiwa ni mgao maalumu wa vitanda 15, magodoro 15 na mashuka 60," alisema Dkt. Kondo.

No comments