Header Ads

ad

Breaking News

WAKAZI DAR ES SALAAM WAPIMA MACHO BURA

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Patrice Justine akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyejitokeza kupima wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali hiyo katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 17.


Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inafanya upimaji wa magonjwa ya shinikizo la damu, sukari na moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Upimaji huo ujulikanao kwa jina la Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Services umeanza kufanyika leo katika Hosptitali ya JKCI Dar Group na utamalizika kesho Mei 17, 2024 kwa kutoa huduma bila gharama kwa wananchi wote watakaojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Baraka Ndelwa alisema upimaji huo unafanyika ili kuwapa nafasi wananchi kuufahamu vizuri ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na namna ambavyo wanaweza kujikinga na ugonjwa huo.

Dkt. Baraka alisema upimaji huo unatolewa bila gharama ili kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini kufanyiwa uchunguzi, kupatiwa matibabu na wale watakaohitaji dawa kupatiwa bila gharama.

“Tunazishukuru kampuni za dawa za binadamu zilizoshirikiana nasi katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani kwa kuwaletea wagonjwa wetu dawa bila gharama,” alisema Dkt. Baraka

Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Paulina Lwegeta alisema hakujua kama ana tatizo la shinikizo la juu la damu lakini kwasababu ndugu yake ana tatizo hilo na amelazwa katika hospitali JKCI Dar Group akaamua naye atumie nafasi aliyopata kuchunguza afya yake.

“Kupitia matokeo niliyoyapata hapa naona watu wengi tutakuwa tunaumwa ugonjwa wa shinikizo la juu la damu lakini hatujui, natoa wito kwa wananchi wenzangu kuwa na tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara,” alisema Paulina.

Paulina alisema amekuwa akiumwa kichwa kwa muda mrefu lakini hakujua kama ana tatizo la shinikizo la juu la damu hadi leo alipofanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na tatizo hilo ambapo amepatiwa dawa.

Omary Seif mkazi wa Temeke alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu na kupatiwa matibabu katika hospitali tofauti bila ya mafanikio.

“Nimekuwa nikitibiwa tatizo la shinikizo la damu tangu mwaka 2022 katika hospitali tofauti lakini chaajabu hakuna siku presha yangu imeshuka na kukaa sawa, siku zote ipo juu hadi imeniletea matatizo ya macho kwani sasa hivi sioni vizuri”, alisema Omary

Omary alisema baada yakuona matangazo ya upimaji unaofanyika JKCI Dar Group alichukua hatua yakufika katika upimaji huo ambapo amepata huduma na kushauriwa vizuri kuhusu dawa alizokuwa anatumia hapo awali.

Naye, Meneja kutoka kampuni ya dawa za binadamu ya Hetero Lab Ivan Edmund alisema kampuni mbalimbali za dawa za binadamu kwapamoja zimeungana kushirikiana na JKCI kuwapatia wananchi watakaokuta na matatizo ya shinikizo la damu, sukari na magonjwa ya moyo dawa bila gharama.

Ivan alisema kulingana na hali za wananchi wengi kampuni yake na nyingine zilizojitokeza hazikuona shida kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani na wananchi watakaojitokeza kupima katika kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanyika JKCI Dar Group.

“Tunaishauri jamii iache matumizi ya dawa bila ya kumuona daktari ni vizuri kabla ya kutumia dawa ukamuona daktari akakufanyia uchunguzi na kukuandikia dawa sahihi kwani dawa ni tiba na wakati mwingine dawa inaweza kuwa sumu isipotumika vizuri,” alisema Ivan.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Masanja James akizungumza na mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali hiyo katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 17.

 Mwakilishi kutoka kampuni ya dawa za binadamu ya Sun Pharma Oresta Mwila akimhudumia mwananchi aliyepatiwa matibabu katika kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya JKCI Dar Group katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo  Mei 17.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika foleni ya kupatiwa matibabu wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya JKCI Dar Group katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Mei. Picha zote na JKCI

No comments