Header Ads

ad

Breaking News

Unitar yawajengea uwezo wanawake na vijana 50 kufikia taasisi za kifedha


Na Mwandishi Wetu

JUMLA ya wanawake na vijana 50 wa Tanzania wamenufaika na mafunzo ya biashara ya kilimo yanayoendeshwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti (Unitar), yenye maskani yake jijini Geneva nchini Uswisi kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Benki ya Kiarabu ya Uchumi na Maendeleo kwa Afrika (BADEA), yanalenga kuongeza kasi ya Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabia nchi na Kuhuisha Biashara za Kilimo Ndogo na za Kati kwa Wanawake na Vijana.

Akizungumza leo Mei 27,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo hayo ambayo yalianza tangu Novemba 2023 kwa njia ya mtandao, Ofisa wa Mradi wa Unitar, Bw. Michael Adalla, amesema mradi huyo umeendeshwa katika nchi tatu za Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Bw. Adalla amesema kwamba, jumla ya wanufaika 150 kutoka nchi hizo wamejengewa uwezo wa kufikia taasisi za kifedha ili kupatiwa fedha za kuanzisha na kuendeleza biashara zao ndogo na za kati za kilimo ili kufikia malengo yao waliyojiwekea.

Amesema kwamba, mafunzo hayo yamefikia hatua ya washiriki kuomba fedha kwa taasisi za kifedha ambapo kwa upande wa taasisi za fedha maafisa wa CRDB walikuwapo kusikiliza miradi ya washiriki hao inayohusiana na biashara za Kilimo.

Amewataka wanufaika hao ambao wanahitimisha mafunzo yao kesho kuwa mabalozi wazuri na kuwahamasisha wanawake na vijana kushiriki katika kuendeleza biashara zao ndogo na za kati za kilimo.

Bw. Adalla amesema Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti (Unitar), itaendelea kufuatilia biashara zao hizo zinavyoendelea kwa kuzirekodi na kuzihifadhi kwa ajili kumbukumbu kwa manufaa ya wengine.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wanufaika wa mradi wa awali Unitar, Bi. Angelamercy Battazary Baruti anayejihusisha na Kilimo cha Inzichuma kwa ajili ya chakula cha mifugo na kusaidia kuchakata taka zitokanazo na mimea na mifugo pamoja na Beatrice Henry Awino kwa sasa anajishughulisha na kilimo mseto cha ufugaji samaki na kilimo cha mbogamboga.

Wanufaika hao ambao sasa wamekuwa wakufunzi kwa wengine baada ya kujengewa uwezo na Unitar walipata fursa ya kutoa michango yao ya kujengea na kuimarisha miradi ya wanufaika wapya wa kuongeza kasi ya Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabia nchi na Kuhuisha Biashara za Kilimo Ndogo na za Kati kwa Wanawake na Vijana.



No comments