Header Ads

ad

Breaking News

SHINYANGA, MWANZA KUSHIRIKIANA NA TAWA KUPAMBANA NA WANYAMA WAKALI

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Beatus Maganja akisalimiana na mmoja wa wakazi wa Kanda ya Ziwa


Na Beatus Maganja

WANANCHI wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Shinyanga na Mwanza wameahidi kushirikiana na Serikali kukabiliana changamoto ya wanyama wakali ili kupunguza adha kwa wakazi wanaoishi pembeni ya hifadhi.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),  katika mikoa ya Kanda ya ziwa, wananchi hao wameeleza adha kubwa wanayoipata kutokana na changamoto itokanayo na wanyamapori hao ya kuhatarisha maisha yao na kudhoofisha shughuli za kiuchumi.

Wananchi hao wameipongeza TAWA kwa hatua yao ya kuwashirikisha wananchi katika zoezi zima la kukabiliana na changamoto hiyo.

"Kumekuwa na malalamiko mengi kutokana na wimbi la wanyamapori hatarishi, hususani fisi na wengine ambao wamekuwa wakishambulia watu, watoto hushindwa hata kwenda shule na kuwa changamoto kubwa," amesema Leonard Mayala, mkazi wa Kahama

"Lakini ujio wa TAWA umekuwa faraja kubwa kwetu, wamekuja kushirikiana na wananchi ili kukabiliana na changamoto hii ya wanyamapori, wananchi tuko tayari kushirikiana na taasisi hii kwani usalama ni wetu."

"Taasisi hii imekuja na huu mpango kwa ajili ya  salama wetu, hivyo wananchi tunaahidi kutoa ushirikiano kwa TAWA pamoja na kutoa mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori hao," ameongeza.

Naye, Robert Wilson mkazi wa Wilaya ya Misungwi Kata ya Mbarika, ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha Wagalu ameeleza kufurahishwa kwake na lengo la Serikali kupitia TAWA ya kuwashirikisha wananchi kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuahidi kutoa ushirikiano katika mapambano hayo ili jamii iwe na amani.

Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Nyanda amewapongeza wananchi kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kukabiliana na changamoto hiyo, na kwamba ushirikiano huo unatoa mwelekeo mzuri katika kutatua changamoto inayowakabili wananchi hao.

Amesema kutokana na ukubwa wa nchi yetu na upungufu wa rasilimali, ni dhahiri TAWA peke yake haitaweza kuwepo kila mahali hivyo, ushiriki wa wananchi katika uhifadhi na mapambano dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu ni muhimu katika kufikia malengo ya uhifadhi wa wanyamapori nchini.

Maganja amesema TAWA inathamini maamuzi yaliyofanywa na wananchi hao, huku akitoa rai kwa watanzania  kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikizingatiwa kuwa, jukumu la kulinda raia na mali zao ni la wananchi wote.













No comments