Header Ads

ad

Breaking News

POLISI WAKAMATA WATUHUMIWA WANNE WAKISAFIRISHA PUNDA NJE YA NCHI

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi- Longido.

JESHI la Polisi kikosi cha kupambana na kuzuia wizi wa mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha wamewakamata watuhumiwa wanne pamoja na mifugo aina ya punda 46 wakisafirishwa kinyume na taratibu kwenda nje ya nchi.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi linawashirikilia watuhumiwa wanne waliokuwa wakisafirisha mifugo aina punda ipatayo 46 kwenda nje ya nchi kinyume na taratibu.

SACP Pasua amesema kuwa, watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku akibainisha kuwa, majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na kwamba pindi upelelezi utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma zao.

Kamanda Pasua ameongeza kuwa, tayari serikali kupitia wizara ya Mifugo na Uvuvi ilitoa maelekezo juu ya katazo la kusafirisha punda na mazao yake kutokana na kupungua kwa idadi ya wanyama hao, huku akiweka wazi kuwa jeshi hilo litaendelea kuwakamata wale wote watakaobainika kuhusika na usafirishaji wa punda kwenda nje ya nchi.

Aidha, amesema jeshi hilo litaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwakamata wale wote watakaokaidi agizo la serikali la kutosafirisha punda na mazao yake kwenda nje ya nchi kutokana na kupungua kwa idadi ya mifugo hiyo aina ya punda.








No comments