NACONGO WAANZA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA BARAZA
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMATI ya Mpito ya Kuratibu Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACONGO), imetoa wito kwa viongozi na wanachama wa Mashirika hayo, kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Baraza hilo kuanzia ngazi ya wilaya, makundi maalum, mkoa hadi taifa.
Wito huo ulitolewa Mei 16,2024 Jijini Dar es Salaam, na Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya kuratibu uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Christina Ruhinda wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) ambapo amesema kwa mujibu wa kanuni ya 5(a), 5 (b) (ii) na 5(c)(v) ya kanuni za uchaguzi za Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2016, Baraza linawataka kufanya uchaguzi Kila baada ya miaka mitatu.
Ruhinda amesema sifa za mgombea wa nafasi za uongozi ni pamoja na kuwa kiongozi au mwanachama katika Shirika lisilo la Kiserikali lililosajiliwa chini ya Sheria ya mashirika yasiyo ya Kiserikali na mwenye uzoefu na uelewa mpana wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya Mashirika hayo.
“Mgombea awe Mtanzania isipokuwa kwa mwakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa, lakini awe mwenye kibali cha kufanya kazi Tanzania, awe na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 70, asiwe alishawahi kupatikana na makosa ya jinai, awe na elimu ya kidato cha nne au zaidi, awe na uwezo mzuri wa kuzungumza lugha ya Kiswahili na Kiingereza pia awe na akili timamu.” Amesema Ruhinda.
Kuhusu vigezo vya Shirika Kushiriki katika Uchaguzi, amesema kuwa Shirika linatakiwa liwe limesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Sura ya 56 ya Sheria za Tanzania, lakini pia liwe linatekeleza shughuli zake katika eneo husika.
Sambamba na hilo, amesema Shirika liwe katika orodha ya Msajili Msaidizi wa Halmashauri/Wilaya au Mkoa husika, liwe linatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia Mashirika yasiyo ya Kiserikali, ikiwemo ulipaji wa ada na uwasilishaji wa taarifa, na kwamba Shirika lisilo la Kiserikali lililokidhi vigezo vilivyatwa litakuwa na kura moja.
Mbali na hayo Ruhinda ameongeza kuwa zoezi la kuchukua na kurudisha fomu za maombi katika ngazi ya Kila Wilaya na Mkoa litaanza aaa mbili kamili asubuhi na kumalizika saa tisa alasiri, ambapo fomu ya maombi ya kugombea nafasi ya Baraza itatolewa bure na msimamizi wa uchaguzi.
Mgombea atakosa sifa ya kupigiwa kura endapo yatabainika hakujaza fomu za maombi kwa usahihi na ukamilifu, kutokuwa na vitambulisho vinavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, lakini pia kutokuwa na sifa za msingi zilizoainishwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi.
Akizungumzia Kampeni za uchaguzi huo, Ruhinda amesema kuwa wagombea watanadi sera zao kwa wapiga kura katika kila mkutano wa uchaguzi na zoezi la upigaji kura litafanyika kwa Siri.
“Wapiga kura ni wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yaliyokidhi vigezo, Wagombea wataonesha barua ya uthibitisho kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali wanayowakilisha na nakala ya cheti cha usajili, Wagombea katika ngazi ya Mkoa ni wawakilishi watatu waliochaguliwa katika ngazi ya Wilaya, Wagombea katika ngazi ya Taifa ni wawakilishi wa Baraza waliochaguliwa katika kila Mkoa wakiwemo Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa na Makundi Maalum.
“Uchaguzi wa Makundi Maalum utahusisha Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayotekeleza atua za Watu Wenye Ulemavu, Vijana na Watoto”
Aidha, amebainisha kuwa kila mgombea atakuwa na mwakilishi wake atakayehakiki kura za mgombea wake, na mgombea ataandika maelezo na kuyawasilisha kwa msimamizi wa Uchaguzi ikiwa hajaridhia matokeo.
No comments