Header Ads

ad

Breaking News

MWANANCHI SENGEREMA ATUMIA ELIMU YA TAWA KUJIOKOA MDOMONI MWA MAMBA

Mkazi wa Kijiji cha Kasenyi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Obeid Francis (kushoto), akielekea Ziwa Victoria kumwonesha Afisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Beatus Maganja, sehemu ambayo alikamatwa na mamba na kufanikiwa kujikoa


Na Beatus Maganja

MKAZI wa Kijiji cha Kasenyi kilichopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Obeid Francis (44) amenusurika kuliwa na mnyamapori aina ya mamba baada ya kuikumbuka na kuitumia elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu.

Elimu hiyo inaendelea kutolewa na maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), maeneo mbalimbali nchini.

Akisimulia kisa hicho, Obeid amesema tukio la kukamatwa na mamba lilitokea Oktoba 25, 2023 katika Kijiji cha Kasenyi saa 1 usiku, akiwa anaoga pembeni ya Ziwa Victoria, ambapo ghafla alishtukia amekamatwa mkono wa kushoto na mamba na kutupiwa ndani ya maji yenye kina kirefu na baadaye kuibuliwa.

Kwa maelezo yake, kitendo cha mnyama huyo kumwibua na kumrudisha majini kilirudiwa mara kadhaa, huku akitafuta namna ya kujiokoa, ambapo alikumbuka elimu inayotolewa na maofisa wa TAWA inayoelekeza kumchoma jichoni mnyama huyo kwa kutumia kidole, mtu akiwa amekamatwa na mamba.

Alisema mara baada ya kufanya hivyo, mamba huyo aliruka na kupotelea majini na yeye alijikokota kutoka majini akiwa amejaa majeraha.

"Nikiwa naoga majini, wakati ninageuka kwenda kuvaa nguo zangu ghafla nilishtukia upande wa mkono wa kushoto kama kitu kikali kimenirukia kitu kizito na kinene, nilishtuka kikaanza kunizamisha ndani ya maji, nilipata hofu kubwa, fikra zilinituma kwamba hapa tayari nimekamatwa na mamba," alieleza Obeid Francis.

"Aliponiibua akaanza kunipeleka umbali wa hatua tano kwenye maji marefu, roho ikaniambia Sasa nimekufa, sasa nifanyeje? Usiku umeanza kuingia, lakini roho nyingine ikaniambia huwa wanasema mamba ukimkamata macho hukuachia, nilifanya hivyo na kweli akaniachia," alisema.

Matukio ya wananchi kupata madhara yatokonayo na wanyamapori wakali na waharibifu hasa waishio pembeni mwa maziwa na mito yamekuwa yakitokana na vitendo vya wananchi hao kufanya shughuli zao karibu na maji kama kuoga, kufua na uvuvi usio rafiki, mambo ambayo yamekuwa yakihatarisha maisha yao.

TAWA imekuwa ikifanya jitahada endelevu za kutoa elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu, hususan mamba na viboko maeneo mbalimbali nchini.

Lengo la TAWA ni kuhakikisha wananchi anakuwa mbinu za kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na wanyamapori hao na huwasisitiza wananchi kuzingatia elimu hiyo ili waendelee kuwa salama.

Mkazi wa Kijiji cha Kasenyi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Obeid Francis akielezea jinsi alivyojiokoa mdomoni mwa mamba kwa kutumia elimu waliyopewa na maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)
Mkazi wa Kijiji cha Kasenyi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Obeid Francis akionesha kwa mbali sehemu aliyokuwa akioga na kukamatwa na mamba, lakini akafanikiwa kujiokoa

No comments