Header Ads

ad

Breaking News

DKT. ABBAS ATETA NA VIONGOZI TANAPA, AWAPONGEZA KUSIMAMIA VIZURI UHIFADHI NA UTALII


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas,


Na Andrew Charles, Arush

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, Mei 3,2024 alitembelea Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), na kuzungumza na uongozi wa Makao Makuu na Kanda ya Kaskazini.

Katika kikao chake na Menejimenti, Dkt.Abbas aliwapongeza viongozi wa Shirika kwa kuendelea kusimamia vyema shughuli za Uhifadhi na Utalii katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa hapa nchini.

Aliwaeleza wahifadhi kuwa, mbali na changamoto wanazokabiliana , bado wanayo nafasi ya kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo ili kuziwezesha Hifadhi za Taifa kuwa maeneo bora zaidi ya kutembelewa na watalii wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, ameipongeza TANAPA kwa jitihada inazoendelea nazo za kutangaza vivutio vilivyopo pamoja na kuwapokea watalii na kuwapa huduma zinazokidhi viwango.

“Katika idadi ya watalii waliotembelea nchini, tunatambua kuwa mchango wa TANAPA ni mkubwa katika kuifikia idadi hiyo, hongereni sana,” alisema Dkt. Abbas.

Dkt.Abbas alisema kuwa, Mei 2,2024 alitembelea Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya miaka miwili ya filamu maarufu ya “Tanzania: The Royal Tour” na kupokea taarifa ya utendaji kazi ya hifadhi hiyo.

Aliongeza kuwa, zipo baadhi ya changamoto ambazo Kamishna wa Uhifadhi na timu yake ni lazima kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa, changamoto zilizopo katika Mlima Kilimanjaro zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu ili kuongeza kiwango cha watalii kuridhika na huduma na pia watalii hao waendelee kuwa mabalozi wazuri wa vivutio vilivyopo hapa nchini.

Dkt.Abbas aliisisitiza menejimenti ya TANAPA kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii imejijengea heshima kubwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo ni vema heshima hiyo ikalindwa kwa kufanya kazi kwa bidii, uzalendo, uadilifu, kujituma na ubunifu wa hali ya juu.

“Wakati huu ni kipindi ambacho kila mtumishi anapaswa kuweka juhudi katika kutoa ushauri wa kibunifu ili kutatua changamoto zilizopo na pia kuboresha mazingira ya Hifadhi za Taifa,” alisema Dkt. Abbas.




No comments