Header Ads

ad

Breaking News

TCB YAZINDUA KAMPENI YA TOBOA NA KIKOBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo akipeperusha bendera ya Toboa na Kikoba baada ya kuzindua huduma mpya ya Kikoba Kidigitali leo Alhamisi Mei 9,2024, jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo amezindua kampeni ya Toboa na Kikoba ambayo itaviwezesha vikundi mbalimbali vya kuweka na kukopa fedha (Vikoba) kufanya kazi zao kidigitali.

Katika uzinduzi uliofanyika leo Alhamisi Mei 9,2024 jijini Dar es Salaam, aina mbili za vikoba zimezunduliwa, ya kwanza itakuwa ikihusisha watumiaji wa mitandao ya simu ikiwemo Tigo, Halotel, Airtel na Vodacom, wakati aina nyingine ya kikoba ikiwa na uwezo wa kubeba watumiaji wa mitandao tofauti kikipewa jina la Kikoba Mix.

Mihayo amesema kuanzishwa kwa kikoba Mix kunaondoa changamoto ya awali waliyokuwa wakikutana nayo baadhi ya wana kikundi wasiokuwa na namba ya mtandao husika ambayo kikundi chao kimetengenezewa.

Hali hiyo iliwafanya kuwa na uwezo wa kujiunga lakini walishindwa kuchangia michango yao moja kwa moja kutokana na mfumo kutowaruhusu.

“Uzinduzi wa kikoba hiki unakuja katika wakati ambao watu wanatamani kuwa na uwezo wa kuamua namna na wakati wa kufanya miamala yao, njia hii ni salama kwa uwazi na inawezesha kufanya miamala kwa haraka,” amesema Mihayo.

Amesema uendeshaji wa kikoba mix na kikoba cha kawaida unasimamiwa na TCB chini ya miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania hivyo inafanyika kwa kufuata misingi iliyowekwa na Serikali.

“Niwatie imani kuwa wateja wetu wote waliojiunga kupitia vikundi hivi kuwa fedha zao zitakuwa salama, hili limeanzia hapa lakini itakwenda nchi nzima ili watanzania waweze kuelewa kampeni ya hii ya toboa na kikoba ni nini, namna ya kujiunga na kikundi na imekuja na utaratibu mzuri wa kuwawezesha kila mtu,” amesema Mihayo.

Sonia Tuteka ambaye ni ambaye ni katibu wa kikoba cha Good Hope amesema awali matumizi ya laini tofauti yalikuwa kikwazo kufikia huduma za kikoba kidigitali tofauti na sasa ambapo kila mwanachama bila kujali mtandao aliopo anaweza kufikia huduma hizo.

“Tulikuwa tukikusanya zile hela tunakubaliana tufanye kitu lakini tunashindwa kupata muafaka kwa sababu huyu ana laini hii, mwingine, Airtel, mwingine Halotel inakuwa changamoto tofauti na sasa,” amesema Sonia.

Anelisya Mwakamelo ambaye ni mwenyekiti wa Bodaboda Millenium Tower II amesema kwa sasa bodaboda zaidi ya 20 ambao wamejiunga katika kikoba ili waweze kufurahia matunda yaliyomo.


No comments