Header Ads

ad

Breaking News

DC SUMAYE AHAMASISHA WATANZANIA KUPIGIA KURA MLIMA KILIMANJARO, SERENGETI

Na Philipo Hassan, Kilimanjaro

MKUU wa Wilaya ya  Moshi vijijini, Zephania Sumaye amewataka watanzania kuupigia kura Mlima Kilimanjaro unaowania tuzo za World Travel Awards 2024 katika kipengele cha Africa’s Leading Tourist Attraction. 

Mkuu wa wilaya huyo aliyasema hayo katika hafla ya kutoa vyeti kwa vijana maarufu kama Ramadhan Brothers washindi wa tuzo za America’s Got Talent 2024 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kupeleka tuzo zao katika kilele cha Uhuru na kuhamasisha kampeni maarufu kama 'Vote Now' mahsusi kwa ajili ya kuzipigia kura Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Serengeti, hafla hiyo ilifanyika Mei 4, 2024 katika ofisi za makao makuu ya Kampuni ya Zara Advanture, Moshi Kilimanjaro.

Alisisitiza kuwa, “Tuupigieni kura Mlima wetu mwaka huu upate kushinda tuzo hizi za kimataifa, Mlima ni wetu, upo kwetu lazima tupende vya kwetu.”.

Sumaye aliwapongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Ramadhan Brothers na Kampuni ya Utalii ya ZARA Advature kwa kuratibu na kufanikisha zoezi zima la kuwapeleka Ramadhan Brothers Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuutangaza na Kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutangaza Utalii wa Tanzania.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Jully Lyimo kutoka TANAPA aliwapongeza Ramadhan Brothers na kuwasisitiza wawe mabalozi wa vivutio vyetu. 

“Mtakavyokuwa mnashiriki matamasha makubwa duniani mtakuwa na fursa ya kuuelezea vizuri Mlima Kilimanjaro kwa sababu mmeupanda na mmejionea uzuri wa mlima mrefu barani Afrika na Mlima uliosimama peke yake duniani.”

Watanzania wote tuendelee kupigia kura Hifadhi ya Kilimanjaro na Serengeti ili ziweze kuibuka kidedea katika tuzo za World Travel Awards na kuendelea kupanua wigo wa kutambulika kimataifa sababu ambayo itaongeza chachu kwa watalii kuzidi kuamini maeneo yetu na kuzidi kutembelea nchi yetu ya Tanzania.













No comments