Header Ads

ad

Breaking News

DC KYERYA ASEMA TANAPA NI WASHIRIKI WAKUBWA KUWAKABILI WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU


Na Brigitha Kimario, Kyerwa

MKUU wa Wilaya ya Kyerwa, Zaituni Msofe amelishukuru Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kupitia Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha pamoja na kuwasaidia wananchi waliopo jirani na hifadhi wanapovamiwa na wanyama wakali na waharibifu.

Ameyasema hayo Mei 21, 2024 katika hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti na vitendea kazi vijana 12 waliohitimu mafunzo ya kujilinda na wanyama wakali katika Chuo cha Pasiansi Mwanza.

"Nawashukuru sana wahifadhi wa Ibanda-Kyerwa na Rumanyika- Karagwe, wamekuwa wepesi sana kuwasaidia wananchi pindi wanapopatwa na kadhia ya kuingiliwa na wanyamapori wakali katika maeneo yao, tumekuwa tukishirikiana vizuri kuhakikisha wananchi wanakuwa salama."

"Mmeona ni vyema kuwasaidia vijana hawa kupata mafunzo ya kukabiliana na wanyama waharibifu ili waweze kutoa taarifa na huduma mapema kabla wahifadhi hawajafika, kwa kufanya hivyo kutapunguza uharibifu wa mazao na vifo vinavyotokana na wanyamapori hao."

DC Msofe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi unaoendelea katika Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyerwa kwa kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo.

"Serikali inatupenda sana wakazi wa Kyerwa, tukipita kule tunaona kuna mambo yanaendelea hasa ujenzi wa lango la kukusanyia mapato pindi watalii wanapoingia (Complex gate), nyumba za watumishi, pamoja na kuboresha mtandao wa barabara, hii itasaidia sana watalii wanapofika kwetu wanapita na kuona wanyama," amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Ibanda- Kyerwa na Rumanyika-Karagwe, Afisa Uhifadhi Mwandamizi, Goliath Mtawa ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na uongozi wa vijiji kwa ushirikiano wao na kutoa vijana ili wapate mafunzo yaliyowajengea weledi wa kukabiliana na wanyamapori hao, sanjari na kutoa taarifa za ujangili ndani na pembeni mwa hifadhi hizo ili kulinda rasilimali kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Mhitimu wa mafunzo hayo, Festo Domitiani kwa niaba ya wahitimu wenzake, ametoa shukrani za dhati kutokana na mafunzo waliyopata na kuomba mafunzo hayo yaendelee kwa vijana zaidi ili kuongeza nguvu kazi na kuimarika kwa utendaji kazi katika vijiji vilivyopo mbali.

Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kujenga makazi au kulima karibu na maeneo ya hifadhi ili kuepuka hatari zinazoweza kutokea kutokana na wanyama wakali na waharibifu kama tembo, nyati, kiboko na mamba.







No comments