Header Ads

ad

Breaking News

CCBRT YAADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA KUTOKOMEZA FISTULA, WAELEZA MAFANIKIO YAO

Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya CCBRT, Dkt.Francis Mchomvu,


Na Mwandishi Wetu

MAADHIMISHO ya Siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula ya uzazi hufanyika kila mwaka ifikapo Mei 23, ambapo mwaka huu wa 2024 inaadhimishwa jijini Arusha, lengo likiwa ni kuhamasisha jamii, kupanua wigo wa kuhudumia wagonjwa wa fistula , kuimarisha ubia na kuweka Pamoja rasimali za kukabiliana na tatizo la ugonjwa huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Dkt.Daniel Michael, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya kina Mama Hospitali ya CCBRT, amesema hospitali hiyo ni mdau mkubwa katika mapambano dhidi ya fistula hapa nchini, hivyo wanaungana na wadau wenzao huko Arusha, wanawake wanaoendelea na matibabu hospitali hapo Pamoja na watoa huduma wao wanaoadhimisha siku hiyo na kupeana taarifa mbalimbali juu ya changamoto za ugonjwa huo.

Dkt.Michael amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, Hospitali ya CCBRT imefanya upasuaji wa kina mama wenye shida ya fistula 1,350, lakini kwa kipindi cha mwezi wa kwanza hadi wa nne mwaka huu wa 2024 wagonjwa wa fistula wapatao 126, wamefaniwa upasuaji Hospitali ya CCBRT.

Naye, Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya CCBRT, Dkt.Francis Mchomvu, amesema fistula ni tundu lisilo la kawaida kati ya uzazi na kibofu cha mkojo au njia ya haja kubwa, ambalo husababishwa na uchungu wa muda mrefu na uzazi pingamizi wakati wa kijifungua bila msaada wa haraka.

"Mama mwenye fistula ya uzazi hutokwa na haja ndogo au kubwa, wakati mwingine  vyote kwa pamoja ,kupitia ukeni bila kuwa na uwezo wa kujizuia, hali ambayo humdhalilisha  na kumfanya ashindwe kushiriki ikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii na wakati mwingine kutengwa na mume au familia.

Eva Ndala, moja wa wanawake wenye fistula alioko hospitalini hapo, amesema alipopata ugonjwa huo ambao amekaa nao muda wa miaka miwili, alinyanyapaliwa sana na jamii inayomzunguka pamoja na kutelekezwa na mume wake.

Bi.Ndala ameishukuru Hospitali ya CCBRT kwa msaada wa matibabu anayopata, baada ya baada mmoja kufika nyumbani kwake na kujitambulisha kama balozi wa fistula katika eneo lao, akamweleza uwepo wa matibabu ya bure ya ugonjwa huo.

Amesema alimsafirisha hadi Hospitali ya CCBRT, ambako aliwakuta wanawake wengi wenye tatizo hilo, wakiendelea kupata matababu katika hospitali hiyo yenywe wataalam waliobobea kwa matibabu ya ugonjwa huo.

"Mimi nimeshatibiwa, ni mzima wa afya, nasubiri kuruhusiwa kurejea nyumbani, naushukuru sana uongozi wa Hospitali ya CCBRT kwa huduma bora inayotolewa na wafanyakazi wote," amesema.

Maadhimisho Siku ya Kimataifa ya kutokomeza Fistula, mwaka huu imebebwa na kauli mbiu isemayo 'Vunja Mnyororo, Zuia Fistula Tanzania', kauli mbiu hiyo inaweka msisitizo mkubwa wa kuzuia fistula kwa kukabiliana na mapungufu kwenye mifumo ya afya na kwenye jamii ambayo husababisha uzazi pingamizi ambacho ni chanzo kikubwa cha ugonjwa huo.

Dkt.Daniel Michael, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya kina Mama Hospitali ya CCBRT



No comments