Header Ads

ad

Breaking News

CARIBBEAN NAPLES ZOO YAISAIDIA MAGARI MAWILI HIFADHI NGORONGORO

Ngorongoro Kreta, Arusha

TAASISI ya Caribbean Naples Zoo kutoka nchini Marekani imetoa msaada wa magari mawili kwa mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi wa faru na wanyama wengine katika hifadhi hiyo.

Mkurugenzi wa Caribbean Naples Zoo, Tim Tetzlaff amesema taasisi yao ni wadau wa shughuli za uhifadhi, baada ya kutembelea Tanzania miaka ya nyuma kwa shughuli za utalii walifurahishwa na juhudi za uhifadhi wa wanyamapori hasa faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa magari mawili.

“Sisi ni wadau wakubwa wa shughuli za uhifadhi na kwa mara ya kwanza tulikuja Tanzania kwa shughuli za utalii, taasisi yetu ikafurahishwa na uhifadhi hasa wa faru na wanyama wengine katika Hifadhi ya Ngorongoro, hivyo kutoa magari haya mawili kunalenga kuunga mkono juhudi za Serikali na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika uhifadhi endelevu,” amesema Tetzlaff.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Elirehema Doriye ameishukuru taasisi hiyo na kuahidi kuwa NCAA kupata magari mawili, taasisi hiyo imeongeza nyenzo kwa askari wa uhifadhi katika ulinzi wa faru na wanyama wengine na kusaidia kuongeza uhifadhi na utalii katika Kreta ya Ngorongoro.

“Hifadhi ya Ngorongoro ndiyo eneo pekee lenye wanyama adimu kama faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili, tumeendelea kuwalinda, kuwatunza na kuwahifadhi ambapo idadi yao inaendelea kuongezeka, kupata magari mawili kwa wadau wa Caribbean Naples Zoo kumeongeza nguvu kwa askari wetu kupata vitendea kazi muhimu katika shughuli za ulinzi wa kila siku,” ameongeza Dkt. Doriye.





No comments