Header Ads

ad

Breaking News

BABU TALE AGAWA MITUNGI YA GESI KWA WAPIGA KURA

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana (kulia), akikabidhi jiko la gesi kwa mkazi wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo hilo, Hamisi Taletale (Babu Tale)


Na Mwandishi Wetu, Ngerengere

MITUNGI 800 ya gesi ya Kampuni ya Oryx Gas Tanzania ikiwa na majiko yake, imetolewa bure kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mitungi hiyo imetolewa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Oryx na mbunge wa jimbo hilo Hamisi Taletale (Babu Tale), katika mkutano mkuu wa CCM Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki mgeni rasmi akiwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana.

Akizungumza kabla ya kukabidhi mitungi hiyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Kinana amempongeza Mbunge Taletale kwa kushirikiana na wadau kugawa mitungi hiyo kwa wananchi hao kwani ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesisitiza kuwa, Rais Samia ameanzisha kampeni ya nishati safi yenye lengo la kumtua mzigo wa kuni mwanamke na hatimaye kumpa muda mwingi katika kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo hasa kwa kutambua mwanamke ndiyo nguzo ya familia.

“Kampeni hii ya nishati safi ni matokeo ya sera na ubunifu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mwaka jana alianzisha mchakato wa kuwatua kina mama mzigo wa kuni.

"Hivyo, katika kufanikisha kampeni hiyo Serikali peke yake haitaweza kwasababu inahitaji fedha nyingi, hivyo nikupongeze Taletale kwa kuunga mkono jitihada za Rais katika kampeni hii, kwani tutakabidhi mitungi ya gesi kwa wananchi, lakini niwapongeze wadau wa gesi kwa kushiriki katika kufanikisha kampeni hii yenye lengo la kumtua mzigo wa kuni mwanamke,"amesema Kinana.

Wakati huo huo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania, Benoite Araman, Meneja wa Mifumo ya Gesi yenye Matumizi Makubwa Oryx Gas Tanzania LTD, Richard Sawere amesema hatua ya kushirikiana na Mbunge Taletale kugawa mitungi hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia.

Amesema Rais Dkt.Samia amedhamiria ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya watanzania wawe wananatumia nishati safi ya kupikia huku akifafanua Kampuni ya Oryx pia umeamua kunusuru uharibifu wa mazingira na kulinda afya za wananchi kwa kutumia nishati safi na rafiki kwa afya za wananchi.

"Nchini Tanzania, wananchi 33,000 wanapoteza maisha kila mwaka kwa kuvuta moshi na chembe chembe zinazotokana na mkaa na kuni. Kupika na gesi ya Oryx itatatua jambo hili," amesema.

Awali, akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitungi na majiko hayo, Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Peter Ndomba amesema sera ya kampuni hiyo ni kuhakikisha nchi nzima inatambua umuhimu wa kutumia gesi.

"Hii ni kampeni ya kitaifa ambayo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliizindua kwa lengo la kuhakikisha kwamba, miaka 10 ijayo zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi."

Katika hatua nyingine, Mbunge wao amesema Rais Samia ameelekeza kutekelezwa kwa kampeni ya nishati safi, hivyo wana Morogoro Kusini Mashariki wameona kuna kila sababu ya kumuunga mkono Rais Samia kwa vitendo kwa kutumia nishati safi ya kupikia inayotokana na gesi ili kuachana na kuni na mkaa.




No comments