Header Ads

ad

Breaking News

TUTAENDELEA KUSIMAMIA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI-WAZIRI NAPE

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye akielezea uhuru wa vyombo vya habari katika mkutano wa kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jumatatu Aprili 29,2024.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye amesema Serikali itaendelea kusimamia waandishi wa habari na vyombo vyao vya habari kufanya kazi kwa utulivu, bila kubugudhiwa na mtu yeyote ili mradi havivunji sheria na taratibu ambazo zimewekwa.

Waziri Nape amesema kuwa, katika eneo la uhuru wa vyombo vya habari nchini mambo yanakwenda vizuri, kwani waandishi na wahariri wanaandika habari bila woga wala hofu ya kitu chochote wakifuata misingi ya sheria zilizopo. 

Amesema hali hiyo haikutokea hivi hivi, ni kazi kubwa na uamuzi wa dhati alioufanya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan wa kuamua kwa makusudi vyombo vya habari viwe huru na kutoa mchango mkubwa katika kukuza utawala bora na utawala wa sheria nchini.

"Nikiri nimeguswa na kaulimbiu ya mkutano huu wa 13 wa Kitaaluma, inayosema “Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu.” Sote tunafahamu kuwa, Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kuwa Kinara wa Uhamasishaji wa Matumizi ya Gesi Barani Afrika, kaulimbiu hii imenigusa na nimefurahishwa na nia ya Jukwaa la Wahariri Tanzania kuamua kwa dhati kuunga mkono matumizi ya gesi ya kupikia majumbani.

Waziri Nape amewataka wahariri katika mwaka huu wa Kitaaluma waliouanza, waone habari nyingi zinazoeleza faida ya matumizi ya gesi, wawaondoe watu hofu juu ya matumizi ya gesi, lengo likiwa ni kuokoa misitu. 

Amesema wanashukuru kuona Wahariri wanatambua mabadiliko ya sheria waliyofanya kwa Kashfa kuiondoa kwenye ujinai, na wataendelea kuboresha sheria kadri hali inavyoruhusu, huku akiomba vyombo vya habari vifanye kazi kwa weledi mkubwa kitaaluma. 

"Kimsingi tunavipongeza vyombo vya habari ambavyo hadi sasa hatujaona matukio makubwa ya kukatishana tamaa, vyombo hivi vinafanya kazi nzuri kwa sasa, ambayo tunavisihi viendelee nayo," amesema Waziri Nape.

Amesema wanafahamu taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na baadaye mwakani Uchaguzi wa Serikali Kuu, hivyo anavisihi vyombo vya habari vijikite katika kujenga hoja kwa kuchapisha na kutangaza habari zilizosheni ukweli bila upendeleo wala uonevu.

Ameongeza kuwa, vyombo vya habari vitoe nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa na wagombea wote, hali itakayoionesha dunia kuwa, hakika Tanzania inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari kwa dhati.

Kuhusu kuanzishwa kwa taasisi zinazotajwa kwenye Sheria ambazo ni pamoja na Bodi ya Ithibati (Accreditation Board), Baraza Huru la Habari (Independent Media Council) na Mfuko wa Mafunzo (Media Fund), amesema ipo mezani kwake.

Amesema taasisi hizo zilipaswa kuundwa hata kabla ya marekebishao ya sheria ambayo yamefanyika mwaka jana, huku akisisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hizo na ndiyo maana zimewekwa kwa mujibu wa sheria.

Waziri Nape amesema mchakato wa kuunda taasisi hizo upo katika hatua ya juu kabisa, na si muda mrefu vyombo hivyo vitaanzishwa.

Kuhusu uwezeshaji wa vyombo vya habari kiuchumi, Waziri Nape amesema kuwa, ni kweli hali ya kiuchumi ya vyombo vyetu vya habari si nzuri kabisa, hali hiyo ndiyo iliyomsukuma kuunda Tume ya kulifanyia kazi suala hili. 

"Tume imekamilisha kazi tuliyoituma. Imekuja na mapendekezo mazuri mno, ambayo serikali tunajipanga kwa utekelezaji wake. Hili la kuzitaka wizara kutenga bajeti ya kutosha ya matangazo, hatuna mgogoro nalo, tutazihimiza kwani tunaliona ni muhimu. Tutazungumza na wenzetu kuwashauri katika wizara na idara mbalimbali watenge bajeti ya kutosha itakayowawezesha kulipia huduma za matangazo kwa wakati pale wanapopata huduma hiyo," amesema Waziri Nape. 

Waziri Nape ameipongeze Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), kwa hatua iliyoichukua kuhakikisha taasisi za umma zinakutana na wahariri na vyombo vya habari kueleza kazi zinazofanya.

Amesema katika muktadha wa kuendesha mambo ya nchi kwa uwazi, amewawaeleza wahariri kwamba, ni jukumu la ofisi za umma kutoa taarifa kwa vyombo vya habari pale zinapohitajika kwa mujibu wa sheria, hivyo tayari wakati wote kutoa taarifa kwa umma kila wanapotakiwa kufanya hivyo.





No comments