Header Ads

ad

Breaking News

TEF YAHAMASISHA MATUMIZI YA GESI KULINDA MISITU

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza katika mkutano maalum wa kitaaluma wa wahariri Jumatatu Aprili 29,2024 jijini Dodoma


Na Mwandishi Wetu

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko kwa kufungua mkutano wa kitaalum wa wahariri wenye kauli mbiu 'Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu.'

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema kuwa,Jukwaa la Wahariri Tanzania linakuwa na mikutano miwili ambayo wa kitaaluma na Mkutano Mkuu unaofanyika kati ya Oktoba na Novemba kila mwaka.

Balile amesema kuwa, Mkutano wa Kitaaluma (Retreat), hutumiwa na wahariri kupitia kazi za kitaaluma walizozifanya, uhai wa taaluma, mazingira ya kazi, matatizo na fursa zilizopo katika jamii tunayoifanyia kazi na kupendekeza suluhisho. 

Amesema mkutano huo hujiwekea malengo ya jinsi ya kutimiza wajibu wao kitaaluma katika mwaka unaouanza kitaaluma, wawe na ajenda zipi kama vyombo vya habari kwa ajili ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, utulivu, umoja na maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

Mwenyekiti wa TEF amesema kuwa, kauli Mbiu hiyo imebeba ujumbe unaozingatia kwamba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Novemba mwaka jana, alichaguliwa kuwa Kinara (Champion) wa Ajenda ya Nishati Safi na Salama ya Kupikia kwa Wanawake wa Afrika katika mkutano wa COP28 uliofanyika nchini Dubai.

Amesema wameona ni bora vyombo vya habari navyo vishiriki kuunga mkono nia hiyo njema ya Rais Samia na hasa suala la nishati linaloangukia katika Wizara yako.

"Tumebaini kuwapo kwa dalili za rasilimali ya gesi kutotumika ipasavyo kutatua changamoto hasa katika sekta ya nishati, kwa maana ya upatikanaji wa umeme nchini na kutumiwa kama nishati safi ya kupikia kwa kina mama, licha ya kujengwa bomba la kusafirisha rasilimali hiyo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, ambalo ujenzi wake uligharimu mabilioni ya shilingi," amesema Mwenyekiti wa TEF.

Amesema bomba hilo kwa taarifa zilizopo linatumika kwa kiwango cha chini kwani miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi iliyopo Kinyerezi, Dar es Salaam haijafanya kazi kwa idadi ya megawati zilizokusudiwa. 

"Tuliahidiwa Kinyerezi I, II, III na IV, lakini taarifa tulizonazo, Kinyerezi III na IV hazijafanya kazi kwa kiwango kilichokusudiwa."

Amesema awali walielezwa kuwa, nyumba nyingi za watu binafsi zingeunganishwa katika mfumo wa gesi asilia na kutumia nishati hiyo kupikia ambayo ina nafuu kubwa ikilinganishwa na nishati nyingine. 

Amesema waliaminishwa kuwa, vituo vya mafuta nchini vingeunganishwa na nishati hiyo ya gesi asilia, ambapo gharama ya kuendesha magari kwa kutumia gesi ni ya chini mno akitolea mfano mtumiaji wa gari dogo la IST akijaza mafuta lita 40 kwa wastani wa shilingi 120,000, kwa umbali ule ule, wakati anayetumia gesi atajaza mtungi mmoja kwa shilingi 17,000. 

"Kwasasa Dar es Salaam kuna vituo vitatu vya gesi na Dangote anacho kimoja mkoani Mtwara, lakini mikoa mingine nchini haina kituo hata kimoja," amesema.

Mwenyekiti amesema wahariri wanatamani kuona mchango wa rasilimali gesi katika uchumi wa nchi  na watu wake, na zaidi kusaidia taifa kuondokana na changamoto ya kina mama wenye macho mekundu kutokana na moshi wa kuni kudhaniwa kuwa ni wachawi na kuuawa katika baadhi ya mikoa hapa nchini.

Balile amesema TEF wamekutana jijini Dodoma katika kipindi ambacho kumekuwapo ongezeko la uhuru wa habari, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka minne iliyopita. 

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia imeleta nafuu kubwa katika uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa kukusanyika, kuabudu, kukusanya, kuchakata na kuchapisha taarifa bila kujali mipaka ya nchi. 

Ameongeza kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, wameshuhudia mabadiliko ya sheria yaliyofuta Kashfa kugeuzwa jinai katika vitabu vya sheria vya Tanzania, hiyo ikiwa ni hatua  kubwa na ya kupigiwa mfano.

Mwenyekiti wa TEF amesema tangu mwaka 2016, miaka minane hadi leo, wamekuwa wakisubiri Serikali ianzishe taasisi zinazoanzishwa na sheria hiyo ambazo ni pamoja na Bodi ya Ithibati (Accreditation Board), Baraza Huru la Habari (Independent Media Council) na Mfuko wa Wanahabari (Media Fund) kwani tumevisubiri kitambo vyombo hivi, ambavyo vikianzishwa wanahabari watapumua.

"Kesi nyingi zinazofunguliwa kila kona nchini, sheria hii inataka zipitie kwenye Baraza Huru la Habari, hivyo likiwapo waandishi wataondokewa na vitisho dhidi ya kutumia uhuru wa kitaaluma, kwani katika Mahakama za chini ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, kuna baadhi ya hukumu ni za mkomoeni. Tuna mfano wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, bila mtuhumiwa wala mlalamikaji kuwapo mahakamani na ikatoa tuzo ambayo ni kubwa iko nje ya mipaka ya kisheria. Ni hatari. Tunaomba vyombo hivi vianzishwe haraka."

Amesema Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amekuwa na ushirikiano mkubwa na vyombo vya habari tangu ateuliwe, hivyo wana imani atakamilisha haraka mchakato wa uundwaji wa vyombo hivyo ili vishiriki kuwawezesha wanahabari kujisimamia kama zilivyo nchi nyingi duniani.

Kuhusu uchumi wa vyombo vya habari, Balile amesema Serikali nyingi duniani zimeacha kuua waandishi wa habari, bali zinaua uandishi wa habari kwa kutumia mbinu ya kuvinyonga kiuchumi vyombo vya habari ili visiwe na uwezo wa kulipa waandishi mishahara, posho za wawakilishi (correspondents), bima za afya, kusafirisha waandishi kwenda mikoani na mwisho wa siku waandishi wawe ombaomba. Sauti ya maskini huwa hasikiki popote, isipokuwa akiangua kilio. 

Amesema mwaka 2016, hapa kwetu sheria iliingiza kifungu cha 5(L) kilichokuwa kinaweka mikononi mwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), mamlaka ya kukusanya na kusambaza matangazo kwenye vyombo vya habari kutoka taasisi na idara zote za serikali, matumizi ya kifungu hicho kilionekana.

Ameongeza kuwa, hicho ndicho kilikuwa chanzo cha vifo vya vyombo vya habari nchini, hivyo wanamshukuru Mhe. Rais Samia kukifuta kifungu hicho katika marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2023.

"Wakati yanafanyika marekebisho haya, tayari vyombo vya habari vilishakuwa hoi, Serikali kupitia Wizara na Taasisi zake, ziliacha kutenga bajeti ya kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari, baadhi ya watendaji waliona hatua hiyo inawapa nguvu ya kuvidhibiti vyombo vya habari visipige kelele," amesema.

Amesema wakati huu wa Kipindi cha Bunge la Bajeti, wanaomba Wizara na Taasisi za Serikali zitenge na kuongeza bajeti ya kujitangaza au kutangaza shughuli zao kwenye vyombo vya habari, ambako wengi wanataka kupewa huduma ya matangazo, lakini hawataki kuilipia kwa kisingizio kuwa hawana bajeti. 

Ametolea mfano wizara moja mwaka huu imeyaomba magazeti yatangaze hotuba yake ya bajeti kwa gharama ya shilingi milioni 1, yaani kurasa 10 kwa shilingi milioni moja ambazo kwa bei ya soko ni wastani wa shilingi milioni 40, hiyo ni hatari, inasikitisha.

Kuhusu upatikanaji wa taarifa, amesema hatua hiyo ndiyo msingi wa utendaji wa vyombo vya habari na Serikali ndiye mdau mkubwa wa taarifa ambazo huchakatwa na kuwezesha umma kupata habari za masuala mbalimbali. 

"Tunaomba kutambua na kupongeza hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi alioufanya wa kukutana na waandishi wa habari kila mwezi pale Zanzibar. Ni utaratibu mzuri sana, ingawa naye hatujui kwa nini ameusitisha kwa muda sasa," amesema.

Jukwaa la Wahariri Tanzania lina dhima ya kuilinda, kuitetea, kuheshimisha na kuithaminisha taaluma ya habari mbele ya jamii, kwani ndiyo walinzi wa kweli wa taaluma ya uandishi wa habari nchini.






No comments